1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaanza mkakati wa kupima corona vijijini

Sylvanus Karemera19 Julai 2021

Wakati aina mpya ya kirusi cha Corona- Delta kikiripotiwa nchini Rwanda, serikali ya nchi hiyo imeanza mkakati wa kuwapima wakaazi kuanzia vijijini hadi mjini

Burundi Gasenyi Flüchtlinge kehren aus Ruanda zurück
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Sambamba na hilo pia serikali ya Rwanda inakusudia kutoa vyakula katika familia zilizoathiriwa na agizo la kusalia ndani ambalo limewekwa kwa muda wa siku kumi kuanzia Jumamosi iliyopita kukabiliana na corona.

Serikali ya Rwanda imesema licha ya kuweka agizo la kutotoka nje kwa muda wa siku kumi katika mji mkuu Kigali na katika wilaya nyingine nane zenye maambukizo mengi, bado zoezi la kuwapima wananchi wengi kadri inavyowezekana litasaidia kubaini ni kwa kiwango gani virusi vya Corona vimesambaa nchini humo.

Juhudi za kunyunyiza dawa ya kuua vijiduduPicha: DW

Zoezi hili la upimaji litafanyika kutoka ngazi ya kijiji ambapo wananchi wote wametakiwa kupimwa. Kwa kawaida mwananchi hutakiwa kujigharamia mwenyewe kipimo cha Corona, gharama yake ikiwa ni faranga elfu kumi sawa na dola kumi za Marekani.

Maoni ya wananchi yamekuwa mengi; "Nimefarajika sana kupimwa maana kwa kawaida inakuwa siyo rahisi kupata pesa ya kujigharamia kuchukua vipimo.Bahati nzuri nimekuta bado niko salama lakini hiyo haina maana kukiuka masharti ya kujiepusha na tatizo hili hapana." Mwananchi mwingine alisema kuwa "Corona haichagui yeyote kila mmoja anaweza kuathirika kwa hiyo nimefurahi kwa kuwa nimeweza kupima bure,nahamasisha na wengine kuja kupima maana wanaweza kuathirika pasipo kujua."

Waziri wa afya wa Rwanda Dr. Daniel Ngamije amesema zoezi hili la upimaji linanuia kupata picha kamili ya jinsi virusi vya corona vilivyosambaa nchini.

Rwanda kuwapima corona wananchi vijijini

This browser does not support the audio element.

"Hadi mwishoni mwa zuio la kukaa ndani tutakuwa angalau tumepima watu katika sehemu maambukizi mengi kama vile wilaya 8 na katka mjii mkuu wa Kigali.Lengo upimaji huu ni kupata taswira ya uzito wa tatizo la maambukizi miongoni mwa wananchi.Naili upate majibu sahihi lazima upime idadi kubwa ya wananchi ili iwe sampuli ya mikakati utakayochukua badaaye".

Mkimbizi wa Burundi akipimwa joto nchini RwandaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Wakati huo huo, mapema leo serikali ilianza kutoa mgao wa vyakula kwa familia zilizoathirika kiuchumi kutokana na vikwazo vilivyowekwa vya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19.

Serikali inasema haitaki kuwaacha wananchi wakitaabika. Huyu ni waziri anayehusika na serikali za mitaa JMV Gatabazi.

"Hakuna mwananchi hata mmoja ambaye kwa sababu hajiwezi au kwa kawaida ni maskini ambaye ataathiriwa na hili katazola kutoka nje,hapana, hata yule ambaye kwa kawaida alijiweza lakini kutokana na katazo hili pengine biashara yake au chanzo kingine kikasimama atakosa chakula hapana. Tutajitahidi kuwasaidia maana serikali imejipanga kutekeleza haya yote."

Agizo la kusalia ndani litadumu kwa muda wa siku kumi tangu lilipoanza Jumamosi iliyopita, vipimo vinavyochukuliwa ndivyo vitakavyoamua ikiwa agizo hilo litaendelea kutekelezwa kwa muda zaidi au litaondolewa.

Mwandishi:

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW