1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yadaiwa kuwazuilia na kuwatesa watoto wa mitaani

27 Januari 2020

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema Rwanda inataka kuhalalisha mchakato unaoonekana kuwa wa maonevu wa kuwakamata na kuwafungia watoto wa mitaani kwa kisingizio cha kuwabadilisha tabia.

77 Percent Straßenkinder in Lome Togo
Picha: Marta Rey/Juan Maza

Kulingana na Lewis Mudge  mkurugenzi wa shirika hilo upande wa Afrika ya Kati, Rwanda inadai inawakamata watoto hao kwa nia ya kuwabadilisha tabia, lakini badala yake inawafungia kwa njia isiyokuwa ya kibinaadamu, kuwapiga na kuwaweka katika mateso makubwa.

Ripoti hiyo ya kurasa 44 iliyopewa jina la "ilimradi tunaishi mitaani watatupiga tu, Rwanda yawazuwiya na kuwatesa watoto walioko vizuizini” inaelezea mateso wanayopitia watoto wa mitaani ndani ya miezi sita iliyopita katika  kituo cha Gikondo mjini Kigali.

Huma Rights Watch imewahoji kati ya mwezi Januari na Oktoba mwaka 2019 watoto 30 waliowahi kushikiliwa katika kituo hicho walio na  umri wa miaka 11 hadi 17, pamoja na kuangalia taarifa za umma, nyaraka rasmi, machapisho  katika vyombo vya habari vya serikali, mtandao wa kijamii wa twitter wa maafisa wa serikali, pamoja na taarifa nyengine zilizopatikana katika  tume ya kitaifa ya watoto,Tume ya  kitaifa ya haki za binaadamu na idara ya taifa ya matibabu ya urekebishaji tabia.

Shirika hilo limegundua kuwa mateso yanaanzia mara tu baada ya watoto hao kukamatwa na polisi. Baadhi ya watoto waliripoti kupigwa wakati au baada tu ya kukamatwa. Wengine walizungumzia kupewa taarifa rasmi iliyo na mashtaka dhidi yao, kunyimwa nafasi ya kuwa na wakili, mlezi au mtu wa familia wakati wanapoingizwa katika kituo hicho.

Watoto 28 kati ya 30 waliohojiwa walikiri katika kituo hicho cha Gikondo. "Afisa mmoja alinipiga kwa fimbo kubwa mgongoni mwangu na kwenye makalio wakati nilipowasili huko,”alisema kijana mmoja wa miaka 15 aliyeshikiliwa kwa miezi miwili katika kituo hicho mjini Kigali. 

HRW yataka kituo cha Gikondo kufungwa na uchunguzi wa haraka kufanyika

Lewis Mudge Mkurugenzi wa Human Rights Watch upande wa Afrika ya KatiPicha: Human Rights Watch

Rwanda iliweka sheria  mwaka 2017 inayoielezea Gikondo iliyofunguliwa tangu mwaka 2005, kuwa kituo cha kuwabadilisha tabia watu wakiwemo watoto walio chini ya miaka 18 walio watundu. Lakini Human Rights watch inasema watoto waliokamatwa wanaendelea kupokea mateso katika kituo hicho.

Kulingana na shirika hilo, watoto katika kituo cha Gikondo wanawekwa katika vyumba vilivyojaa watu na saa nyengine kuchangywa pamoja na watu wazima katika mazingira duni kinyume na sheria ya Rwanda na ile ya Kimataifa.  Baadhi ya watoto hutumia godoro na blanketi moja ambazo saa nyengine zinakuwa na chawa na kutofikia huduma za matibabu kwa urahisi.

Hata hivyo Rwanda kupitia waziri wake sheria Johnston Busingye amekanusha yaliyomo katika ripoti hiyo na kusema vituo kama hivyo vinatumika kuwafunza watoto stadi mbalimbali ikiwemo useremala, uchomaji vyuma na kuwabadilisha tabia na kwamba mashirika hayo yanatekeleza kazi zake kwa kuzingatia sheria.

Kwa sasa shirika la Human Rights watch limeitaka Rwanda kukifunga kituo cha Gikondo na kuachana na tabia ya kuwakamata watu ovyo hatua inayosababisha watu kushikiliwa katika vituo vya muda vya kuwazuwiya watu. Rwanda pia imetakiwa kuachana na mfumo wa uonevu na kuubadilisha na ule wa usaidizi lwa wale wanaohitaji.

Shirika hilo pia limependekeza wale waote wanaoshikiliwa katika kituo hicho kuachiwa huru na serikali kuanzisha mara moja uchunguzi hidi ya polisi na taasisi nyengine zinazodaiwa kutekeleza dhukluma dhidi ya wafungwa  wakiwemo watoto na uchunguzi huo unapaswa kuhakikisha kuwa wale waote waliohusika wanafikihswa mbele ya sheria.

Chanzo/Human Rights Watch

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW