1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaendelea kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya kimbari

23 Aprili 2018

Rwanda imewasilisha ombi kwa Uganda, ikitaka kukabidhiwa watuhumiwa 200 wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, wanaoishi Uganda kwa sasa ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Pia imeomba mataifa mengine yaisadie.

Uganda Memorial Genozid
Balozi wa Rwanda nchini Uganda Meja Jenerali Frank Mugambage, akiongoza shughuli ya kuwasha mwenge wa matumaini, katika kumbukumbu ya 24 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, iliofanyika katika kijiji cha Kasensero, wilayani Rukungiri, kusini mwa Uganda, walikozikwa baadhi ya wahanga wa mauaji hayo. (Picha na Lubega Emmanuel).Picha: DW/L. Emmanuel

Balozi wa Rwanda nchini Uganda Meja Jenerali Frank Mugambage ametowa mwito kwa nchi ambazo inadaiwa washukiwa wa mauaji ya kimbari wanaishi, kusaidia katika kuwakamata ili wafikishwe mbele ya sheria.

Akiongoza  maadhimisho ya mauaji hayo ya mwaka 1994, balozi huyo amelezea kuwa ni hatari kwa washukiwa hao kuendelea kuwa huru kwani wanaweza kusambaza chuki zilezile zinazochochea kasumba za mauaji ya kimbari.

Amefichukua kuwa wamewasilisha majalada ya washukiwa 200 walioko Uganda na sasa wanasubiri mwitikio wa serikali ya nchi hiyo kusaidia katika kuwakamata washukiwa hao.

Maadhimisho ya awamu ya 24 ya mauaji hayo kwa upande wa Uganda yamefanyika katika kijiji cha Kasensero ambapo balozi wa Rwanda nchini Uganda meja jenerali Frank Mugambage ametumia tukio hilo kutoa mwito kwa jamii ya kimataifa kusaidia katika kuwakamata watu wanaoshukiwa kuendesha mauaji hayo.

Jamii ya Wanyarwanda walioko nchini Uganda wakiwakumbuka baadhi ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, waliozikwa katika kijiji cha Kasensero, wilayani Rukungiri, kusini mwa Uganda. (Picha na Lubega Emmanuel)Picha: DW/L. Emmanuel

Yasubiri jibu kutoka Uganda

Amelezea kuwa wamekwisha wasilisha kiasi majalada 200 kwa serikali ya Uganda kusaidia katika kuwakamata washukiwa walioko nchini humo. Mabaki ya zaidi ya watu 10,000 imezikwa katika makaburi ya halaiki kwenye maeneo matatu nchini Uganda.

Akitaja makaburi ya halaiki yaliyoko Uganda kuwa kielelezo muhimu kwa ulimwengu kufahamu athari za mauaji ya kimbari, balozi huyo amewasilisha shukurani za serikali yake kwa wanakijiji hasa wavuvi wa Kasensero kwa kujitolea kuopoa milli ya wahanga na kuizika angalau kwa hadhi iliyostahili.

Mahakama maalum ya kimataifa iliendesha mpango wa kuwakamata, kuwafungulia mashtaka na pia kuwahukumu zaidi ya washukiwa 90 wa mauaji ya kimbari katika mahakama iilyokuwa mjini Arusha Tanzania kati ya mwaka 1994 na 2014. Lakini hadi sasa Rwanda ingali inawafuatilia wale ambao inadai hawajafikishwa mbele ya sheria.

Kulingana na takwimu zaidi ya washukiwa 63,000 walihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki tano walipoteza maisha yao, wengine wakitupwa na kufa maji katika mto Kagera. Miili yao baadhi yao ndiyo iliopolewa kwa upande wa Uganda.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW