1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yafungua mpaka kati yake na Uganda

Admin.WagnerD28 Januari 2022

Hatimaye Rwanda imetangaza itaufungua mpaka wa Katuna kati yake na Uganda katika hatua zinazoendelea za kusuluhusisha mzozo wa kisiasa ambao umekuwa ukiendelea kati ya nchi hizo jirani kwa miaka mitano sasa.

Grenze Ruanda - Uganda | Paul Kagame und Yoweri Museveni
Picha: Photoshot/picture alliance

Uamuzi wa huo wa serikali mjini Kigali wa kufungua mpaka huo unafuatia ziara rasmi aliyoifanya nchini Rwanda wiki iliyopita Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mshauri wa masuala ya usalama wa rais Yoweri Museveni wa Uganda, ambaye pia ni mtoto wake. 

Rwanda imetangaza kwamba mpaka huu wa Katuna kati yake na Uganda ambao ulifungwa mwaka 2019 utafunguliwa Januari 31 mwaka huu. Tangazo la wizara ya mashauri ya kigeni ya Rwanda limesema kwamba hatua ya kufungua mpaka inafuatia utekelezwaji wa moja ya maazimio ya kikao cha wakuu wa nchi hizo mbili kilichofanyika katika mpaka huo Februari 21, 2020.

Sikiliza Zaidi: 

Museveni na Kagame wapatana tena

This browser does not support the audio element.

Serikali ya Rwanda aidha imesema baada ya ziara ya Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mshauri wa masuala ya kijeshi wa rais na mkuu wa kikosi cha nchi kavu kule Uganda yaliyoifanya Kigali wiki moja iliyopita, Rwanda ilisema imejidhirisha kwamba kuna hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Uganda kuelekea mstakabali wa uhusiano mwema.

Hata hivyo haikuwezekana mara moja kumpata msemaji wa serikali ya Rwanda kutoa kauli yake, ingawa wiki iliyopita Alain Mukurarinda ambaye ni naibu msemaji wa serikali ya Rwanda alisema hatua zinazochukuliwa na pande hizo mbili ni za kupongeza, lakini alikiri kuwa kurejesha uhusiano wa kisiasa ni mchakato unahitaji muda.

''Naweza kusema kwamba kuna imani kubwa lakini watu wasidhani kwamba matatizo yaliyopo yataisha tu kwa siku mbili, Ikulu ya Rais imetamka wazi siyo siri,ikasema kwamba wamefanya mazungumzo juu ya matatizo yaliyopo na tukakubaliana kuchukuliwa hatua za kusitisha matatizo hayo. Imani ipo lakini watu wasidhani kwamba matatizo hayo yataisha kwa siku mbili kwa sababu ni makubwa.'' alisema Mukururinda.

Lakini wachambuzi wa kisiasa na kisheria wao wamekuwa na maoni tofauti. Dr Alphonse Muleefu ni mchambuzi na mkufunzi wa kitivo cha sheria katika chuo kikuu cha Rwanda.

Dr Muleefu alisema ''Ni miaka miwili sasa tangu mkutano wa mwisho wa marais wa nchi mbili juu ya suala hili. Ninaweza kusema kuwa tunaelekea kuzuri lakini hili litawezekana tu endapo kule Uganda hakutakuwepo tena na watu wanaoharibu mambo. Maana kila hali inapoelekea kutengamaa wale wasiopenda maelewano ya nchi mbili wanazua mengine kule Uganda''

Tizama Video: 

Wakazi wa Katuna walia mpaka wao kufungwa

03:04

This browser does not support the video element.

Rwanda imekuwa ikiituhumu Uganda kuwakamata raia wa Rwanda na watu wengine wenye asili ya Rwanda nchini Uganda kwa madai ya kufanya upelelezi. madai mengine ni kwamba Uganda inawasaidia wapinzani wa serikali ya Rwanda. Kwa upande mwingine Uganda inaishutumu Rwanda kuingilia usalama wake wa ndani kwa kufanya vitendo vya udukuzi na kuufunga mpaka huo.

Sylvanus Karemera- Kigali