1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yafungua tena mpaka na Uganda, miaka mitatu baadae

31 Januari 2022

Rwanda imefungua tena mpaka wake wa ardhini na Uganda Jumatatu, baada ya mpaka huo kufungwa kwa miaka mitatu, hatua inayoashiria kuboreka kwa uhusiano kati ya majirani hao wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Afrika Uganda l Katuna - Grenze zu Ruanda
Picha: DW/A. Gitta

Rwanda ilitangaza uamuzi wake wa kufungua tena mpaka huo wiki iliyopita, kama hatua ya kurekebisha uhusiano ulioharibiwa na tuhuma mbalimbali kutoka pande zote kuhusu ujasusi, utekaji nyara na uingiliaji katika masuala ya ndani.

Hatua ya kufunguliwa mpaka huo imefuatia ziara mjini Kigali, ya mtoto wa rais Yoweri Museveni Muhozi Kainerugaba, ambako alikutana na rais wa Rwanda Paul Kagame.

Soma pia:Rwanda yafungua mpaka kati yake na Uganda

Kivuko kikuu cha Gatuna, maarufu kama Katuna nchini Uganda, kilifunguliwa rasmi usiku wa manane, na usafiri ulitarajiwa kuongezeka kasi kadri siku inavyosogea.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wakishikana mikono wakati wa mkutano kwenye mpaka wa Gatuna-Katuna kati ya mataifa hayo mawiki, Februari 21, 2020.Picha: Photoshot/picture alliance

Hata hivyo mwandishi wa DW Lubega Emmanuel alipotembelea mpaka huo, aliripoti kwamba Rwanda imeweka sharti ambapo inawaruhusu tu raia wake wanaotoka Uganda, watalii na magari ya mizigo kuvuka na kuingia katika ardhi yake.

"Mamlaka ya uhamiaji za Rwanda zinasisitiza kuwa kwa sasa wanaruhusu tu raia wake wanaotokea Uganda, watalii pamoja na magari ya mizigo," alisema Lubega na kutolea mfano wa familia iliyojaribu kuingia Rwanda ilikuhudhuria mazishi ya jamaa yao aliyefariki mwishoni mwa wiki lakini wakakataliwa.

Wakazi wa Katuna walia mpaka wao kufungwa

03:04

This browser does not support the video element.

Museveni na Kagame walikuwa washirika wa karibu katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa mapambano ya kuwania madaraka katika mataifa yao, lakini uhusiano wao ulibadilika na kuwa wa uhasama.

Rwanda ilifunga mpaka wake baada ya kuituhumu Uganda kwa kuwateka raia wake na kuunga mkono waasi wanaotaka kuiangusha serikali ya Kagame.

Soma pia: Uganda yakanusha madai ya Rwanda kuhusu kundi la M23

Uganda nayo ikaituhumu Rwanda kwa kuifanyia udukuzi pamoja na kuwauwa wanaume wawili wakati wa uvamizi ndani ya ardhi ya Uganda mwaka 2019 -- madai ambayo Kigali inayakanusha.

Mtoto wa rais Yoweri Museveni na kamanda wa majeshi ya ardhini Uganda, Jenerali Muhozi Kainerugaba.Picha: DW/E. Lubega

Serikali zote mbili zilisema wiki iliyopita kwamba zilitumai kufunguliwa tena kwa mpaka kutachangia kusawazisha uhusiano.

Kabla ya kufungwa kwa mpaka huo, mauzo ya Uganda nchini Rwanda -- ambayo yanahusisha kwa sehemu kubwa saruji na chakula -- yalifikia zaidi ya dola milioni 211 mwaka 2018, kwa mujibu wa tarakimu za Benki ya Dunia, wakati Rwanda iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 13 nchini Uganda.

Biashara ilishuka mwaka 2019, huku hali hiyo ikichochewa zaidi na mzozo wa Covid.

Chanzo: afpe, Lubega Emmanuel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW