Rwanda yaishitaki Uingereza The Hague
28 Januari 2026
Katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rwanda imewasilisha ilani katika mahakama ya usuluhishi wa mizozo iliyo na makao yake mjini The Hague Uholanzi, ikidai Uingereza imekiuka makubaliano ya kifedha yaliyokuwepo katika mpango huo ambao ulikuwa ushuhudie wahamiaji haramu Uingereza kupelekwa Rwanda.
Rwanda imeongeza kuwa mwaka 2024, Uingereza iliitaka isiyazingatie malipo ya awamu mbili ya dola milioni 69 yaliyokuwa yanastahili kufanywa Aprili 2025 na Aprili mwaka huu 2026, wakitazamia kufutiliwa mbali kwa makubaliano yaliyokuwa kwenye mkataba huo.
Njia ya kidiplomasia kugonga mwamba
Rwanda vile vile inasema ilikuwa tayari kukubali hilo,mradi tu mkataba huo usitishwe na makubaliano mapya ya kifedha yajadiliwe na yafikiwe na kulingana na Kigali, hakukufanyika majadiliano yoyote na Uingereza, kwa hiyo bado inadai kulipwa fedha kama ilivyoafikiwa awali kulingana na mkataba uliokuwepo.
Mshauri Mkuu wa Kiufundi katika wizara ya sheria ya Rwanda Michael Butera, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, walitafuta njia za kidiplomasia za kusuluhisha tofauti hizo zilizopo na Uingereza ila hawakufanikiwa ndipo wakaamua kuchukua hatua za kisheria.
Msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza lakini amesema kuwa Uingereza itajitetea vilivyo ili kuzilinda fedha za wananchi wake walipa kodi.
Chini ya mkataba huo uliotiwa saini kabla Keir Starmer kuingia madarakani, Uingereza ilikubali kuilipa Rwanda kuwachukua wahamiaji ila Uingereza iliishia kuwapeleka wahamiaji 4 pekee, kwani mpango huo ulikumbwa na vigingi vya kisheria.
Kuvurugika kwa mahusiano
Baada ya kuufutilia mbali mpango huo, Starmer alisema kuwa serikali yake ilikuwa imepoteza fedha za umma na kwamba hakuna fedha zengine zitakazolipwa kwa Rwanda.
London ilikuwa imeshailipa Kigali zaidi ya dola milioni 330.
Mahusiano kati ya Uingereza na Rwanda yalivurugika mwaka 2025, pale Uingereza ilipositisha msaada kwa Rwanda kwa dhima yake kwenye vita vya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Rwanda imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kimataifa kutokana na madai kwamba inaliunga mkono kundi la waasi la M23. Kigali inakanusha kuwaunga mkono waasi hao na inaitupia lawama wanajeshi wa Kongo na Burundi kwa mapigano mapya, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu na kuwapelekea mamia kwa maelfu kuachwa bila makao katika mwaka mmoja uliopita.
Vyanzo: Reuters/AFP