Rwanda yajiandaa kwa mashindano ya Baiskeli duniani
15 Septemba 2025
Kufuatia maandalizi hayo serikali imetangaza kuwa shule zitafungwa kwa muda huo na wafanyakazi wa serikali watafanyia kazi nyumbani.
Jiji la Kigali limejiandaa kupokea washiriki mashuhuri wa mbio za baiskeli kutoka sehemu mbalimbali duniani, watakaokuwa wakipita kwenye mitaa na katika ya jiji hilo.
Hii ni mara ya kwanza mashindano haya kufanyika barani Afrika, jambo linalochukuliwa kama hatua kubwa kwa Rwanda na bara zima la Afrika.
Wafanyakazi wa serikali wanaofanya kazi Kigali pia wametakiwa kufanya kazi wakiwa nyumbani au sehemu nyingine kwa kutumia teknolojia, katika kipindi chote cha mashindano, isipokuwa wale wanaotoa huduma muhimu zinazohitaji uwepo wao mahali pa kazi. Mashirika binafsi yenye uwezo pia yameshauriwa kutumia mfumo wa kazi kwa kutumia teknolojia wakati wote wa mashindano.
Msimu mpya viongozi wapya
Tukiwa bado nchini , Ligi kuu ya soka nchini Rwanda msimu wa 2025/26 umeanza mwishoni mwa wiki hii ukiwa na uongozi mpya, Ligi Kuu ya Rwanda imemteua Mkurugenzi Mkuu mpya, Jules Karangwa, huku FERWAFA ikimchagua Shema Ngoga Fabrice kuwa Rais kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Rais mpya wa FERWAFA ameahidi kuongeza zawadi kwa vilabu vya soka nchini.
Mkurugenzi Mkuu mpya, Jules Karangwa akiongea na DW amebaini kuwa hii itaongeza chachu ya ushindani
‘'Unapoongeza zawadi, unaongeza pia sababu nyingine inayochochea vilabu kushindana zaidi na kufanya ushindani uwe mkali. Hivyo basi, kuongeza zawadi kutoka milioni 25 kwa timu iliyotwaa ubingwa wa ligi hadi kufikia milioni 80, tunaamini kutasaidia sana, kwani ni mara ya kwanza kutoa zawadi kwa timu 6 za mwanzo kati ya timu 16''
Moja ya changamoto zinazotarajiwa kutatuliwa katika msimu huu wa michezo ni kipato kidogo cha waamuzi, ambapo Rais wa FERWAFA, Shema Fabrice, amewaahidi kuwa posho walizokuwa wakipewa zimepanda mara nne. waamuzi sasa watakuwa wakilipwa Laki moja faranga za Rwanda( Elfu 100 Frw) kwa kila mchezo wanaoamua,
Burundi inahitaji muujiza kufuzu kwa kombe la dunia
Huku haya yakijiri, Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Burundi Intamba mu Rugamba Patrick Sangwa amesema kwamba kupata tikiti ya kufuzu kombe la dunia ni miujiza, baada ya kupata matokea mabaya kwenye michezo miwili iliyopita ya kusaka tikiti ya kombe la dunia.
Kwetu sisi ni miujiza au ndoto ambayo tulikuwa nayo kucheza kombe la dunia, mechi mbili ambazo tumecheza ikiwa ni pamoja na Ivory Coast na Gambia mechi ya Ivory Coast tumepoteza bao 1-0.Mimi nataka kujenga kitu ambacho mwaka kesho wakati tutakapo michuano ya mchujo kuelekea fainali za AFCON 2027 ili tushiriki, hilo ndilo lengo letu. Alisema Sangwa.
Intamba mu Rugamba ya Burundi itakuwa na miadi na Kenya Harambee Stars kwenye mechi ya marudio jijini Bujumbura , Burundi na mechi ya mwisho ya kufuzu fainali za kombe la dunia itafanyika Libreville, Gabon mwezi ujao octoba 2025.
//Christopher Karenzi DW Kigali