Rwanda yakanusha madai ya Burundi kuwapa silaha waasi
13 Mei 2024Taarifa hiyo imetolewa siku moja, baada ya tuhuma za Burundi kwamba Rwanda imewapa mafunzo na silaha waasi wanaolaumuiwa kwa mashambulizi mawili ya guruneti. Watu 38 walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo siku ya Ijumaa mjini Bujumbura.
Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, amekanusha madai hayo, akisema "hayana uhusiano kabisa" na shambulio hilo. Makolo amesema, Burundi ina tatizo na Rwanda, lakini wao hawana tatizo na Burundi. Aidha, serikali ya Rwanda imewatolea wito viongozi wa Burundi kutatua matatizo yake ya ndani bila kuihusisha Rwanda.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili jirani, mara umekuwa wa kupanda na kushuka. Mara kwa mara, Burundi imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao. Madai ambayo yamekanushwa na Serikali ya Rwanda na pia kundi hilo la Red-Tabara.