1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yakiri kupoteza askari wanne huko Cabo Delgado

29 Septemba 2021

Kwa mara ya kwanza tangu Rwanda ilipotuma vikosi vyake katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji nchi hiyo imethibitisha kuwapoteza askari wake 4 na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Ruanda Mosambik Militär
Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Mwezi wa saba Rwanda ilituma Kikosi cha askari mchanganyiko wa polisi na jeshi wapatao 1000 kwenda kwenye jimbo hilo kushirikiana na jeshi la Msumbiji kupambana na magaidi waliolidhibiti jimbo hilo kwa zaidi ya miaka minne na kusababisha vifo vya mamia ya raia wasiokuwa na hatia. 

Taarifa ya kuuawa kwa wanajeshi wanne wa Rwanda nchini Msumbiji ilithibitishwa na msemaji wa jeshi la Rwanda kwa waandishi wa habari hata hivyo bila ya kunaswa sauti. Hii imekuwa ni mara ya kwanza Rwanda kutangaza habari kuhusu kuuawa kwa wanajeshi wake ambao kwa ushirikiano na jeshi la Msumbiji wamekwisha likomboa jimbo la Cabo Delgado nchini humo ndani ya kipindi cha miezi miwili na nusu iliyopita.

Hata hivyo alipovitembelea vikosi vyake mjini Pemba ambao ni mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado mwisho mwa wiki iliyopita Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuthibitisha idadi ya vifo vya askari wake.

Rais Paul Kagame na mwenzake wa Msumbiji Filipe NyusiPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Taarifa zimeeleza kwamba idadi kubwa ya magaidi imeendelea kuuawa na baadhi kukamatwa huku wananchi waliokuwa wametoroka makazi yao katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Cabo Delgado kurejea makwao. Taarifa za kupoteza maaskari wa Rwanda zimeonekana kutotajwa sana kama zile kuhusu ushindi wa majeshi ya Rwanda kulikomboa jimbo la Cabo Delgado.Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa na diplomasia wanaamini licha ya mafanikio ya jeshi la Rwanda bado hakuna kinga juu ya hasara ya vita

Jeshi la Rwanda limekuwa likitangaza maeneo kadhaa yanayoendelea kukamatwa na kwa upande mwingine Rais Kagame anasema kama ambavyo majeshi ya nchi mbili yalivyoshirikiana kuwakabili magaidi hao pia yatashirikiana kuzihudumia familia zilizopoteza wanajeshi hao.

Tayari Rwanda na Msumbiji zimekwishatia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi ukiachilia mbali ule wa ushirikiano katika ulinzi na usalama wa nchi mbili.

Mwandishi:  Sylivanus Karemera