1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yakumbuka robo karne ya mauaji ya kimbari

Yusra Buwayhid
5 Aprili 2019

Jumapili Rwanda itaanza kumbukumbu za miaka 25 za mauaji ya kimbari. Watu 800,000  wengi wao Watutsi walipigwa, na wengine kuuawa katika kipindi cha siku mia moja. Robo karne baadaye nayaliyotokea hayajasahaulika.

Ruanda Gedenkstätte an Völkermord in Nyamata
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Kama ilivyozoeleka, kila Aprili 17 ambayo itakuwa Jumapili kwa mwaka huu - siku mauaji hayo ya kimbari yalipoanza- Rais Paul Kagame atawasha mwenge wa kumbukumbu katika  Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari kwenye mji mkuu wa Kigali ambako inaaminika zaidi ya waathirika 250,000 walizikwa hapo.

Siku hiyo itakuwa ndiyo mwanzo wa kumbukumbu hizo ambazo zitakuwa na matukio kadhaa yatakayodumu kwa siku mia moja zijazo zilizotengwa kusudi kwa maombolezo ya nchi nzima.

Mchana wa siku hiyo hiyo ya Jumapili, Kagame ambaye aliwaongoza waasi waliopambana na wanamgambo na wanajeshi wa serikali na kubaki madarakani kama kiongozi wa taifa tangu wakati huo, ataongoza hafla ya kumbukumbu katika kiwanja cha soka mjini Kigali.

Ingawa miaka 25 imeshapita, lakini yaliyotokea yameacha mabaki yake. Jean-Paul Haguma, ni mwanafunzi wa miaka 26, na anasema mabaki ya mauaji hayo bado yangaliko na kuonekana dhahir katika jamii za nchini humo.

"Tunaishi na matokeo ya mauaji ya kimbari ambapo unakuta baadhi ya watu wametengwa na familia zao au labda hata hawana familia. Wahalifu, waathirika na hata wale ambao hawakuwa wamezaliwa wakati huo, basi wote wanakabiliwa na matokeo sawa," amesema Haguma.

Rwanda ya chini ya uongozi wa Kagame

Rwanda imebadilika tangu mauaji hayo ya kimbari. Kagame ndiye anayesifiwa kwa kusimamia maendeleo ya haraka ya kiuchumi baada ya mauaji kumalizika. Mafanikio yake hayo yalimpatia umaarufu kama kiongozi wa kuigwa. Lakini kila muda unavyosonga mbele, uongozi wake wa mkono wa chuma -- ambao kwa baadhi unaonekana kuwa unahitajika kuhakikisha utulivu -- unakosolewa na wengi wengine.

Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: picture-alliance/C. Ndegeya

Uongozi wa kibabe wa Kagame unaangaliwa na nchi za Magharibi kuwa ni wa kukandamiza uhuru wa kujieleza pamoja na sauti za upinzani nchini humo. Kawaida wapinzani wa Kagame huwa wananyamazishwa au hata kukimbilia uhamishoni.

Kagame alichaguliwa tena kwa muhula mpya wa miaka saba Agosti 2017, kwa takriban asilimia 99 ya kura zote zilizopigwa. Na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa kupitia kura ya maoni ya 2015, huenda yakamruhusu kubaki madarakani hadi 2034.

Lakini pengine mambo yameshaanza kubadilika. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 sasa, anaonekana kuregeza kamba. Pengine ameshatanabahi, na kuanza kujiuliza nani atashika madaraka atakapoondoka yeye. Kuna hata viongozi wa upinzani walionza kuachiliwa huru kutoka vizuizini walipokuwa wamewekwa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid, afp/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef