1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yapokea wakimbizi kutoka Libya

27 Septemba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa limesema kundi la wakimbizi 66 kutoka Afrika limewasili Rwanda kutoka Libya. Ujio wa kundi hilo huenda ukawa ufunguzi wa maelfu ya wakimbizi kuingia huko kufuatia mpango mpya wa rais Kagame.

Erste Flüchtlinge aus libyschen Lagern in Ruanda angekommen
Picha: AFP/C. Ndegeya

Hatua hiyo inatokana na ombi la rais wa Rwanda Paul Kagame mwaka 2017 la kutoa makaazi kwa waafrika baada ya kuibuka ripoti ya mateso, udhalilishaji wa kingono na kulazimishwa kufanya kazi inayowakumba wakimbizi wa kiafrika nchini Libya.

Mapema mwezi huu Rwanda ilitia saini makubaliano kati yake na Umoja wa Afrika na shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kukubali kuwapa hifadhi wakimbizi waliokwama nchini Libya.

Serikali ya Rwanda imesema imejitayarisha kuchukua wakimbizi 30,000 lakini mpango huo utaanza kwa hatua, kuanzia wakimbizi 500 kabla ya kuwafikia wote elfu 30 ili kuizuwia nchi hiyo kuzidiwa na majukumu kwa wakati mmoja.

Shirika la UNHCR liliandika katika mtandao wake wa kijamii wa twitter "wameshawasili” likimaanisha kundi la kwanza linalowajumuisha vijana walio chini ya miaka 18, kina mama na baadhi ya familia tayari wameshawasili nchini Rwanda. Mkimbizi mdogo kabisa katika kundi hilo ni mtoto wa miezi miwili aliyezaliwa na wazazi walio na asili ya kisomali nchini Libya.

Wakimbizi hao kwa sasa watahifadhiwa katika kituo cha muda cha Gashora, kabla ya kupewa makaazi mengine iwapo hawatotaka kurejea nchini mwao. Baada ya kusajiliwa na kupata hadhi ya ukimbizi watapata vitambulisho vya wakimbizi kama ilivyo kwa wakimbizi wengine.

Jamii ya Kimataifa yahimizwa kuiga mfano wa Rwanda kuwaokoa wakimbizi zaidi Libya

Picha: AFP/C. Ndegeya

Kulingana na Olivier Kayumba Rugina katibu mkuu katika wizara ya usimamizi wa hali za dharura nchini Rwanda, shirika la UNHCR litatoa malazi, elimu, vyakula, bidhaa za msingi za afya, na huduma za afya kwa wakimbizi hao.

Msemaji wa UNHCR Charlie Yaxley ameihimiza jamii ya Kimataifa kuunga mkono mpango wa Rwanda na pia kujitokeza na mpango sawa na huo ili kuwaokoa wakimbizi zaidi wanaoteseka nchini Libya.  Huku hayo yakiarifiwa ndege nyengine itakayokuwa na wakimbizi 125 inatarajiwa kuwasili Rwanda mwezi Ujao kati ya tarehe 10 na 12.

Kufuatia maandamano makubwa ya kudai mageuzi yaliofanyika nchini Libya mwaka 2011 na kusababisha kuondolewa madarakani na baadae kuuwawa kwa kiongozi wa muda mrefu nchini humo Muammar Gaddaffi kuliifanya nchi hiyo kuwa kitovu muhimu kwa wakimbizi wa Afrika kupitia taifa hilo na kutumia njia hatarishi kufika barani Ulaya. Umoja wa Mataifa unasema wakimbizi 42,000 kwa sasa wamekwama nchini Libya.

Mataifa ya Mashariki mwa Afrika kwa kawaida yanapongezwa kwa uwazi wa kuwasaidia wale waliopoteza makaazi kufuatia machafuko katika eneo hilo.

Uganda kwa mfano inatoa makaazi kwa wakimbizi 800,000 kutoka maeneo yanayokumbwa na vita kama SudanKusini huku mataifa mengine afrika Mashariki yakiwapokea maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi, Somalia, na kwengineko.

Mwishoni mwa mwaka 2018 eneo hilo lilitoa hifadhi kwa wakimbizi milioni 4 hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW