1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yasaidia waasi kumpinduwa Nkurunziza

Admin.WagnerD5 Februari 2016

Rwanda imewaandikisha na kuwapatia mafunzo ya kijeshi wakimbizi kutoka Burundi miongoni mwao wakiwemo watoto kwa lengo kuu la kumuondowa madarakani Rais Piere Nkurunziza.

Wakimbizi wa Burundi walioko nchini Rwanda.
Wakimbizi wa Burundi walioko nchini Rwanda.Picha: S. Aglietti/AFP/Getty Images

Jopo la wataalamau wa Umoja wa Mataifa lililoandaa repoti hiyo limesema wamezungumza na wakimbizi 18 wa Burundi ambao walitowa ufafanuzi wa kina kuhusu mafunzo yao ya kijeshi waliopatiwa katika kambi ilioko misituni nchini Rwanda.

Repoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya masuala ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema wakimbizi hao wameripoti lengo lao kuu ni kumuondowa madarakani Rais Piere Nkurunziza wa Burundi.

Burundi mara kwa mara imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi kwa lengo la kuipinduwa serikali nchini humo madai ambayo Rwanda inayakanusha.

Mafunzoya kijeshi

Wakimbizi hao ambao walivuka mpaka kuingia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo waliwaambia wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba waliandikishwa kwa ajili ya mafunzo hayo katika kambi ya wakimbizi ya Mahama ilioko mashariki mwa Rwanda hapo mwezi wa Mei na Juni mwaka 2015.

Wanajeshi wa Burundi wakidhibiti hali ya usalama Bujumbura.Picha: picture-alliance/dpa/D. Kuroawa

Repoti inasema kundi hilo la wakimbizi limepatiwa mafunzo ya kijeshi ya miezi miwili na wakufunzi nchini Rwanda ambao baadhi yao walikuwa ni maafisa wa kijeshi wa Rwanda.

Kwa mujibu wa repoti hiyo mafunzo hayo ni pamoja na mbinu za kijeshi na ukarabati na matumizi ya bunduki za rashasha halikadhalika itikadi na kujenga hamasa.Baadhi yao pia walipatiwa mafunzo ya kutumia mizinga, maguruneti mabomu ya kuripua vifaru na kuvurumisha maguruneti kwa kutumia roketi.

Mkono wa jeshi la Rwanda

Kulikuwa na watoto sita miongoni mwa wapiganaji 18 waliopatiwa mafunzo hayo.Wakimbizi hao wamelieleza jopo hilo la wataalamu kwamba takriban makundi manne yenye makuruta 100 kwa kila kundi yalikuwa yakipatiwa mafunzo katika kambi hiyo na kwamba yalikuwa yakisafirishwa katika maeneo ya Rwanda kwa kutumia magari ya kijeshi ambapo mara nyingi yalikuwa yakisindikizwa na jeshi la Rwanda.

Jeshi la Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa

Wakimbizi hao pia walionyesha vitambulisho bandia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambavyo vilitengenezwa nchini Rwanda.

Shirika la kimataifa la kutetea wakimbizi lenye makao yake nchini Marekani Refugees International limesema mwezi uliopita kwamba wanaume na wavulana wa Burundi wamekuwa wakiandikishwa kuwa wapiganaji kutoka kambi ya Mahama na wanatishwa iwapo wanakataa.

Madai ya kitoto

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekaririwa akisema hapo mwezi wa Disemba kwamba hakuwahi kuona chembe ya ushahidi kuhusu madai hayo aliyoyaita kuwa ya "kitoto".

Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa/G. Ehrenzeller

Watalamu wa Umoja Mataifa pia waliwahoji raia sita wa Rwanda na saba wa Congo waliokamatwa kwa tuhuma za kusafirisha silaha kwa magendo katika mpaka wa Congo na Rwanda hapo mwezi wa Oktoba na Novemba mwaka jana.

Baadhi ya watuhumiwa hao wamesema silaha hizo zilikuwa zimepangwa zitumiwe kulisaidia kundi la wapiganaji nchini Burundi.Burundi imekuwa katika vurugu tokea Nkurunziza alipotangaza mipango ya kuwania muhula wa tatu hapo mwezi wa Aprili ambapo baadae alishinda katika uchaguzi.Takriban watu 400 wameuwawa tokea wakati huo na wengine 230,000 wameikimbia nchi hiyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/AP

Mhariri : Iddi Ssessanga