1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda iko tayari kulipiza kisasi iwapo DRC itashambulia

1 Juni 2022

Kiza kikiendelea kutanda katika mahusiano ya kidiplomasia kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda imesema haitaki kuvutwa kwenye vita lakini haitaendelea kuvumilia uchokozi wa kurushiwa mabomu na DRC

Feierlichkeiten zum Tag der Streitkräfte in Mosambik
Picha: Estácio Valoi/DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dkt Vincent Biruta amelilaumu jeshi la MONUSCO la Umoja wa Mataifa kwa kufumbia macho uchokozi huo huku likishirikiana na waasi wa FDLR wenye itikadi za mauaji ya kimbari na lengo la kuipindua serikali ya Rwanda. Akizungumza na waandishi habari mjini Kigali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Dr Vincent Biruta amesema Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo lilirusha mabomu nchini Rwanda tarehe 19 na 23 mwezi jana, lakini Congo haijaomba msamaha.

Biruta amesema kuwa Congo inataka kuwavuta kwenye vita yao kwa kuwarushia mabomu kila wakitaka. Ameongeza kwamba waliwauliza kulikoni lakini hawajakiri kosa na wala hawajawaambia hatua walizochukua kusitisha uchokozi huo. Biruta pia amesema kwamba wanataka amani, hawataki vita na hawafahamu kwanini Congo inataka vita.

Felix Tshisekedi - Rais wa DRCPicha: Tobias Schwarz/REUTERS

Tofauti zilianzia wapi?

Uhusiano wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliingia doa hasa yalipoibuka mapigano mapya kati ya Jeshi la Congo na waasi wa M23 ambao Rwanda inadaiwa kuwafadhili, huku Rwanda nayo ikiituhumu Congo kwa kulifadhili kundi la FDLR lenye lengo la kuipindua serikali ya Rwanda. Rwanda imesema endapo Congo itaendeleza uchokozi wake na kukataa kuwaachia wanajeshi wawili wa Rwanda inaowashikilia ambao Congo inasema walikamatwa wakiwa wameivamia huku Rwanda ikisema walitekwa nyara wakati wakishika doria mpakani, Rwanda itajibu mapigo.

Biruta ameendelea kusema kwamba wana jukumu la kuwalinda wananchi wao na mipaka yao na kuongeza kuwa nchi ikivamiwa inajitetea. Waziri huyo ameongeza kusema kwamba wana haki kama ilivyo kwa nchi zingine zote na  endapo usalama wao utaendelea kuhujumiwa watajilinda. Aidha Dr Biruta amelilaumu jeshi la Congo FARDC na lile la MONUSCO la Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na waasi wa FDLR katika vita dhidi ya M23 ilhali FDLR ni moja ya makundi ambayo wana jukumu ya kuyasambaratisha.

Katika kutafuta suluhisho la amani katika  mgogoro huu, rais wa umoja wa nchi za eneo la maziwa makuu ICGLR, Joao Laurenco ambaye pia ni Rais wa Angola jana alifanya mazungumzo na Rais Etienne Tshisekedi wa Congo na anatarajiwa kuzungumza pia na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

 

-----

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW