1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda yasema Jumuiya ya Kimataifa inakuza mzozo wa DRC

6 Desemba 2022

Waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda ameituhumu Jumuiya ya Kimataifa kwa kuutanua mzozo wa Mashariki mwa Congo baada ya Marekani kuiomba nchi yake kusitisha kile alichokiita shutuma za kuwaunga mkono waasi wa M23.

Ruanda | Besuch US-Außenminister Antony Blinken
Picha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincet Biruta, amesema rais Paul Kagame wa Rwanda na Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken walikuwa na majadiliano mazuri wakati walipizungumza kwa njia ya simu siku ya Jumapili, lakini bado kulikuwa na tofauti ya kuelewa hasa mzozo uliopo.

Amesema mtazamo mbaya na potofu wa Jumuiya ya Kimataifa unaendelea kutanua tatizo lililopo  huku akiongezea kuwa kuingiliwa kwa mzozo wa congo na mataifa ya nje kunadhoofisha juhudi za kidiplomasia za kutatua tatizo hilo. 

Rwanda imeendelea kuilaumu serikali ya Congo kwa mzozo wa Mashariki na kuituhumu Jumuiya ya kimataifa, kufumbia macho uungaji mkono wa serikali hiyo kwa kundi la FDLR lililopo Congo linaloitishia Kigali. Biruta amesema wasiwasi wa Usalama wa Rwanda ni lazima uzingatiwe. Amesema M23 haipaswi kufungamanishwa na Rwanda na uwepo wao sio tatizo la Rwanda kutatua.

Maandamano ya kushinikiza amani DRC

01:44

This browser does not support the video element.

Siku ya Jumapili Blinken, alimpigia simu rais Kagame akisema ni Lazima Rwanda iache kuwaunga mkono waasi wa M23. Rwanda hata hivyo imeendelea kukanusha mara kwa mara shutuma za kuwaunga mkono waasi wa M23, zinazotolewa na Marekani na hivi maajuzi kuungwa mkono pia na wataalamu wa Umoja wa Mataifa. 

Kundi hilo la waasi linalotokea kabila la tutsi lilianzisha tena mapigano yake Mashariki mwa DRC mwaka 2021 baada ya kusitisha uasi miaka kadhaa. Mashambulizi yake hivi karibuni yamesababisha mgogoro mkubwa Mashariki mwa Congo.

Juhudi za kuumaliza mgogoro huo zinafanyika mjini Nairobi kati ya maafisa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na makundi kadhaa ya waasi upande wa Mashariki lakini sio kundi la M23.

Serikali ya DRC yadai M23 imewauwa watu 272 mjini Kishishe

Picha: Benjamin Kasembe/DW

Wakati huo huo serikali ya Congo imesema watu 272 waliuwawa mjini Kishishe upande wa Mashariki mwa nchi hiyo na kuingeza idadi hiyo ambayo awali litangazwa kufikia 50. Serikali inalilaumu kundi la M23 kwa mauaji hayo jambo ambalo kundi hilo la waasi limekanusha.

Huku hayo yakiarifiwa watu 16 wameuwawa na wengine 25 hawajulikani waliko baada ya kutokea mashambulizi ya kikabila Magharibi mwa Congo.

Malumbano yaendelea baina ya Kongo na Rwanda

Nyumba kadhaa zilichomwa moto katika mji wa Misia mkoani Kwilu  hii ikiwa ni kulingana na waziri wa ndani wa Congo Jean-Claude Bwanganga. Bwanganga amesema tayari polisi na wanajeshi wamepelekwa katika eneo husika kuwasaka waliotekeleza mauaji hayo.

Mapigano kati ya kabila la Yaka na Teke yamekuwa yakiendelea huko tangu mwezi wa sita mwaka huu kufuatia masuala ya arshi na kodi. Watu 180 wamepoteza maisha yao tangu mgogoro huo ulipoanza.

Chanzo: afp/reuters