1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yatahadharisha juu ya mkataba wake na DR Congo

19 Septemba 2025

Serikali ya Rwanda imetishia kuwa mikataba ya Doha na Washington kwa ajili ya kutatua mzozo wa mshariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huenda isifanikiwe.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Rwanda imedai kuwa hali hiyo imetokana na jitihada za serikali ya Kinshasa kutatiza mikataba hiyo. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe ameyasema hayo mjini Kigali akitaja kwamba mienendo ya serikali ya Kongo ya kusuasua katika mikataba unatishia mafanikio yake.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa usiku wa kuamkia Ijumaa, waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe amekumbushia nafasi na faida ya kuwepo kwa mikataba ya Doha na Washington kwamba ni kuhakikisha yanafanyika mazungumzo ya dhati ya kurejesha ustahimilivu wa eneo zima la mashariki mwa Congo na nchi nzima ya Congo.

Hadi sasa kunaendelea mazungumzo mjini Doha nchini Qatar kati ya kundi la waasi wa M23 na serikali ya Kinshasa kuhusu kusitisha mapiganona kwa upande mwingine kunaendelea mchakato wa amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mjini Washington na wiki iliyopita Rais wa Marekani Donald Trump alikumbushia kuwa anatarajia miezi ijayo kuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Congo.

Rwanda: Mienendo ya Kinshasa itakinzana na na mafanikio ya mkataba

Hata hivyo wakati juhudi hizo zote zikiendelea Rwanda imeonya kwamba mienendo ya serikali ya Kinshasa kwa sasa huenda ikakinzana na mafanikio mazima ya juhudi za mikutano hiyo. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe akasema

Rwanda yadai wanaona mashambulizi zaidi kwa Wanyamurenge na katika maeneo yanayomilikiwa na kundi la M23Picha: UPI Photo/Newscom/picture alliance

"Wameleta ndege ndogo za vita maarufu kama drones, bunduki za mizinga, wameleta zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Burundi, wameongeza idadi nyingine ya mamluki kutoka Colombia wanaofanyia kazi kampuni ya Black water inayomilikiwa na raia mmoja wa Marekani anayeitwa Eric Prince, kumbuka hawa ni tofauti na mamluki wa zamani kutoka Romania ambao tuliwapa njia ya kupita hapa kuelekea kwao Ulaya baada ya kushindwa kule mashariki mwa Congo," amesema Nduhingirehe.

Nduhingirehe ameongeza kusema kuwa wakati hayo ni kinyume na mkataba wa kimataifa wanaona mashambulizi zaidi kwa Wanyamurenge na katika maeneo yanayomilikiwa na kundi la M23, lakini mbaya zaidi ni kwamba wanaona kundi la wanamgambo linalojulikana kama Wazalendo lililoanzishwa na serikali ya Kongo na ambao wanaua raia wa Kinyamurenge na Watutsi wa Kongo wanaendelea na machafuko yao.

Waziri huyo amesema hayo yote yanafanyika kwa msaada wa serikali ya Congo huku ikijua fika kwamba kuna mikataba ya amani inayopaswa kutekelezwa. Kuendelea kwa vitendo hivyo dhidi ya raia wa Congo wanaonyimwa haki yao kwa kuitwa raia wa Rwanda ni hatari kwa mchakato wa amani.

Waziri wa mashauri ya kigeni Congo Patrick MuyayaPicha: DW

Wachambuzi wasema shutuma hizo huenda zikaharibu zaidi mchakato wa amani

Hata hivyo wadadisi wa masuala ya kisiasa katika kanda ya maziwa makuu hususan baina ya Rwanda na Congo wanasema shutuma kama hizi huenda zikaharibu zaidi mchakato huu wa amani.

"Ukiangalia mikataba ya Doha na Washington ni mizuri,lakini ukianza kuona upande mmoja unaushutumu mwingine ninaanza kupoteza matumaini ikiwa njia hii ya amani itawezekana kupatikana," amesema Gahizi John, raia wa Rwanda ambaye ni mkaazi wa Kigali.

Rwanda imesema taarifa kuhusu wasiwasi huu imeishawafahamaisha wapatanishi katika mazungumzo hayo kwa sababu hadi sasa kunaendelea mauaji dhidi ya raia wasio na hatia huku serikali ya Kinshasa ikiwakingia kifua wanaofanya mauaji hayo.

Hata hivyo waziri wa mashauri ya kigeni Congo Patrick Muyaya mwezi uliopita alisikika akiilaumu Rwanda kwa mara nyingine tena kuivamia nchi yake kwa maslahi mapana ya kiuchumi, suala ambalo hadi sasa Rwanda inalikanusha vikali.