Rwanda yatakiwa kuheshimu Uhuru wa Kujieleza
5 Juni 2014Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia ilitoa taarifa zenye ushahidi kwamba waandishi habari wamekuwa wakitishwa katika nchi hiyo ya Afrika ya kati na kwamba serikali imeshawahi kukata mawasiliano ya simu katika kipindi cha habari kwenye redio moja nchini humo.
Marekani kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nchi za nje Marie Harf imesema wale waliozuiliwa hawapewi nafasi ya mawasiliano. Hata hivyo serikali ya Rwanda imeanza hivi karibuni kuwapeleka mahakamani baadhi ya wafungwa.
Bi Harf amesema wanaitaka Rwanda kuheshimu uhuru wa watu kujieleza wakiwemo waandishi habari ili waweze kuchunguza, kuripoti na kuanzisha mijadala tofauti juu ya masuala yanayohitaji kuangaziwa na umma.
Wasiwasi wa Marekani umetokana na ripoti ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch iliotolewa May 16, na kuelezea kupotea pamoja na kutiwa nguvuni kwa watu kadhaa nchini Rwanda kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Inasemekana baadhi walizuiliwa na jeshi na wanaweza kuwa chini ya ulinzi wa jeshi hilo.
Shirika la Human Rights Watch lilifanya utafiti wake kwa kuwahoji watu takriban 14 lililosema kuwa walikuwa hawajulikani waliko Kaskazini Magharibi mwa wilaya ya Rubavu karibu na mpaka wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kusema kuwa kulikuwa na kesi nyengine za watu kupotea katika eneo la Musanze na katika mji mkuu Kigali.
Kiongozi wa Upinzani aapa kurejea katika siasa Rwanda
Inasemekana baadhi yao waliodhaniwa kuwa miongoni mwa kundi la FDLR ambayo Rwanda inalitaja kuwa kundi la Kigaidi linaloendeleza sera za mauaji ya kimbari.
Aidha Harf amesema Marekani inaunga mkono juhudi za Rwanda za kutaka kuwatambua watu wanaotaka kuanzisha ghasia dhidi ya watu wake au serikali lakini akaonya juu ya kukamatwa na kuzuiwa kwa watu ovyo ovyo.
Huku hayo yakirifiwa kiongozi mmoja wa upinzani aliye mashuhuri nchini Rwanda , Bernard Ntaganda ameapa kurudi katika siasa. Hii ni baada ya Ntaganda kuachiwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka minne gerezani kwa makosa ya kutishia usalama wa nchi.
Ntaganda ambaye ni wakili na muanzilishi wa chama cha upinzani cha PS-Imberakuri alitaka kupambana na rais Paul Kagame katika uchaguzi wa mwaka 2010 lakini akakamatwa na kufungwa kabla ya uchaguzi huo.
Kagame,aliyewahi kuwa kiongozi wa waasi, ambaye jeshi lake liliwaondoa waasi wa kihutu kufuatia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 amekuwa akizidi kukosolewa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na madai ya kuwakandamiza wapinzani pamoja na mauaji ya wapinzani walioko uhamishoni.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri Yusuf Saumu