Rwanda yatangaza usafiri wa bila visa kwa Waafrika wote
3 Novemba 2023Hatua ya kuondoa visa kwa Waafrika wanaosafiri kwenda Rwanda, ilitolewa jijini Kigali na Rais Paul Kagame. Kagame amelitaka bara la Afrika kuwa eneo moja la utalii, huku akisikitishwa kuona kwamba asilimia sitini ya watalii barani Afrika ni kutoka nje ya bara hilo, kulingana na data za Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa.
Akifungua hafla ya mkutano wa kimataifa wa 23 wa baraza la utalii Duniani, Rais Paul Kagame alisema Mwafrika yeyote, anaweza kupanda ndege kwenda Rwanda wakati wowote anapotaka na hawatalipa chochote kuingia katika nchi yake.
Kagame alisema kuwa katika dhamira ya kujenga upya taifa lake kutoka takriban 30 iliyopita, Rwanda ilitambua utalii kama kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi.
''Tulifikiria Rwanda ambayo mtu yeyote ulimwenguni angependa kusafiri kwenda. Hivyo ndivyo, tulichagua utalii mapema na kuufanya kama kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi na ajira. Na hatujakatishwa tamaa.'', alisema Kagame.
''Afrika inapswa kusimulia hadithi zake yenyewe''
Rais wa Rwanda amesema Waafrika ni mustakabali wa utalii wa kimataifa katika miongo ijayo. Kwa upande wake, rais wa Tanzania ambaye pia alihudhiria mkutano huo wa kimataifa wa utalii alitoa wito kwa nchi za Afrika kuandika upya kuhusu bara hilo kwa kueleza simulizi zao wenyewe.
"Afrika inapaswa kusimulia hadithi zake kwa njia yake yenyewe na kuanzisha simulizi chanya kuhusu bara letu. Hatuwezi kumudu kuendelea kukaa kimya katika zama hizi za habari za uzushi.", alisema Samia.
Rais Samia amesema serikali za Afrika lazima zijitafakari upya ili utalii uweze kushamiri ikiwemo kujitanzaga kimkakati, kufanya utafiti na uhifadhi.
Endapo hatua ya rais Kagame itatekelezwa, Rwanda itakuwa nchi ya nne barani Afrika kuondoa vikwazo vya usafiri kwa Waafrika. Nchi nyingine ambazo tayari ziliondoa masharti ya visa kwa raia wa Afrika ni Gambia, Benin na Ushelisheli. Rais wa Kenya William Ruto alitangaza Jumatatu mipango ya kuruhusu Waafrika wote kusafiri katika taifa hilo la Afrika Mashariki bila visa ifikapo Desemba 31.