1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Rwanda yatengeneza mashine yake ya kupumulia

Sylvanus Karemera21 Aprili 2020

Katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 Rwanda imezindua mashine ya kwanza iliyotengenezwa nchini ambayo inawasaidia wagonjwa kupumua maarufu kama ventilator.

Rwanda Kigali | Beatmungsgeräte | Manufaktur in Kigali
Picha: DW/S. Karemera

Ni mashine iliyotengenezwa na vijana wanane wa chuo kikuu cha Rwanda kwa msaada wa wakufunzi wao na lengo likiwa ni kuitua serikali mzigo wa kuagiza mashine kama hizi kutoka nje.

Kwa kawaida mashine hii inayomsaidia mgonjwa aliyeko mahututi kupumua wenyewe wanasema thamani yake ni dola elfu 10 za Marekani inaponunuliwa kutoka nchi za nje.

Hata hivyo mabingwa walioitengeneza wanasema kwamba kwa sasa kutokana na dunia kukabiliwa na tatizo la Covid-19 bei ya mashine hii imepanda hadi dola za Marekani elfu 20.

Profesa Stephen Rulisa mkufunzi katika chuo kikuu cha Rwanda anasema licha ya kuongoza mchakato wa kuitengeneza mashine hii ni vijana wake walioitengeneza.

Sisi tunawapa kazi ya kisayansi, tunawapa mawazo kama haya kisha wao hukaa kwenye maabara kama hapa na tunafurahi kwamba hatimaye wanafanya jambo kama hili," alisema Profesa Rulisa.

Wataalamu wakiifanyia majaribio mashine ya kupumulia iliyotengenezwa nchini Rwanda kwa ajili ya wagonjwa mahututi wa covid-19.Picha: DW/S. Karemera

Wahandisi vijana waliotengeneza mashine hii wanasema haikuwa kazi ndogo lakini iliwezekana na inawezekana kuzitengeneza nyingine nyingi za aina hii, lakini hilo litategemea pale tu serikali itakapowajibika zaidi.

"Tunachohitaji ni ushirikiano wa ngazi zote ili tutengeneza mashine nyingi na kuziweka sokoni kwa sababu zinahitajika kwa wingi," alisema Costa Uwitone, mmoja wa wanafunzi walioshiriki kutengeneza mashine hiyo.

Viwanda vyaanza kutengeneza barakoa

Wakati huo huo pia viwanda nchini Rwanda vimeanza kutengeneza barakoa ambazo serikali inasema kutokana na hilo, iko mbioni kumtaka kila mwananchi kuiva popote anapokuwa ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya taifa ya tiba Dr Nsanzimana Sabin anasema barakoa zina ubora kama zile zinazoingizwa nchini kutoka nje.

"Tunatambua bei ya barakoa na ubora wake kwa kuzingatia afya zetu kama binadamu, hatupendi kutengeneza vitu vyenye viwango vya chini hapana, ila barakoa zina viwango bora na pia bei ambayo kila mmoja anaweza kumudu."

Kwa mara ya kwanza idadi ya wagonjwa wanaopona na kuruhusiwa kutoka imepanda kuliko ile ya wagonjwa wanaoendelea kulazwa.

Siku ya Jumatatu, kati ya vipimo 1299 vilivyochukuliwa hakukupatikana mtu hata mmoja huku watu wanne wakipona na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Mpaka sasa Rwanda ina visa 147 vya corona huku watu 80 wakiwa wamepona na 67 wakiendelea kutibiwa hospitali.


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW