1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yatolea kauli ripoti ya Umoja wa Mataifa

Sylvanus Karemera4 Januari 2019

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilibainisha kuwa makundi yenye silaha yanayopambana dhidi ya serikali ya Rwanda yanapata msaada kutoka Burundi na Uganda. Sasa serikali ya Rwanda imesema haitavumilia uchokozi huo.

Ruanda vor den Wahlen 2017
Picha: Imago/Zumapress/M. Brochstein

Siku moja baada ya ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kubainisha kuwa makundi yenye silaha yanayopambana dhidi ya serikali ya Rwanda yanapata msaada kutoka Burundi na Uganda, serikali ya Rwanda imesema haitavumilia uchokozi huo. Bila kuzitaja nchi za Burundi na Uganda zenye sintofahamu na nchi hiyo, Rwanda inasema inalifuatilia tatizo hilo kwa namna ya kipekee.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dkt. Richard Sezibera, ambaye pia ndiye pia msemaji wa nchi, amesema kwamba kundi lenye silaha la FDLR linaloshutumiwa kuhusika katika mauaji ya Rwanda ya mwaka 1994 likiendesha harakati zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, na lile la RNC la Kayumba Nyamwasa aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi ya Rwanda akiwa sasa uhamishoni nchini Afrika Kusini yanapata misaada ya hali na mali kutoka nchi mbili za kanda ya Maziwa Makuu.

Makundi ya FDLR na RNC yanapata silaha kutoka Uganda na Burundi- UN

Ripoti ya watalaamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu makundi yenye silaha mashariki mwa DRC imesema kwamba makundi hayo mawili yanapata misaada kutoka Burundi na Uganda. Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Richard Sezibera, anasema hilo lina ushahidi usiopingika:

"Rwanda haitoi malalamiko, Rwanda inatoa ushahidi kuhusu usumbufu wa haya makundi, huu ni ushahidi wa majina,mahali walipo, ushahidi wa silaha zinazotumiwa, sisi kama serikali tuna ushahidi huo na tumeshautoa kwa mataifa yanayounga mkono makundi hayo na pia tumeshautoa kwa jumuiya ya mataifa. Hii ni ripoti ya watalaam wa Umoja wa Mataifa na sisi tunatarajia ripoti hii itatolewa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na tunahisi baraza hilo litachukua mikakati kuhusu ripoti hiyo."

Rais Kagame: "Baadhi ya matatizo yetu husababishwa na mataifa jirani"

Hii pia imejiri siku chache baada ya Rais Paul Kagame kutangaza msimamo wake juu ya tatizo hilo, alipokuwa akihutubia taifa kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya: "Uhusiano wetu na mataifa mengine ya kiafrika uko vizuri lakini kuna matatizo yanayosababishwa na baadhi ya mataifa jirani zetu.

Baadhi ya majirani zetu hao wanaendelea na vitendo vinavyonuia kufufua makundi yenye silaha kama vile FDLR na RNC yenye lengo la kuhatarisha usalama wetu. Vitendo hivi hudhoofisha mikakati ya maendeleo ambayo kwa kawaida imekuwa ikiendelea vizuri katika nchi zetu za jumuiya ya Afrika mashariki. Haya yapo ijapokuwa mataifa hayo yanakanusha ukweli huo."

Rwanda imesema kwamba licha ya kuendelea kulizungumzia suala hilo na majirani zake, haitazuia kuweka mikakati mikali kulinda mipaka yake. Hii pia inajiri huku kukiendelea visa vya chini kwa chini vya watu wenye silaha hasa kwenye mpaka wa Rwanda na Burundi.

Mwandishi: Sylvanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW