SADC kuupiga jeki uchumi wa Zimbabwe
17 Oktoba 2008Jumuiya ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika ya SADC,inatafuta msaada wa kiuchumi kwa mmoja wa wanachama wake ambae amezongwa na matatizo Zimbabwe.Msaada huu wa kiuchumi ni sehemu ya juhudi za kanda hiyo kujaribu kuyapiga jeki mapatano ya amani ambayo yanayumbayumba.
Hii ni sehemu ya kwanza ya kuunusuru uchumi wa nchi hiyo ambao unaonekana kama umesambaratika.
Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika ambao walihudhuria sherehe ya kutia saini mkataba wa kugawana madaraka mjini Harare mwezi uliopita, wameitwika mzigo sekreterieti ya SADC kupanga aina ya msaada ya kiuchumi unaofaa Zimbabwe.
Katibu Mkuu Tendaji wa SADC,Thomas Salamao,ambae nae pia alihudhuria sherehe ya mjini Harare na pia kuhusika katika juhudi za kuufufua uchumi wa taifa hilo,ameliambia shirika la habari la IPS kuwa ofisi yake imekuwa inajihusisha kuunda mpango wa kuupiga jeki uchumi wa Zimbabwe tangu mwaka wa 2005.
Hata hivyo hakusema ni kiasia gani cha pesa wanachofikiria pamoja na masharti ya msada huo bali kusema kuwa hilo ni la viongozi wa SADC.
Pia hakusema ni mda gani mpango huo utaanza ama kikomo isipokuwa kukariri kuwa hilo litategemea mapatano ya kuwagana madaraka yatakavyotekelezwa.
Ibara ya tatu ya makubaliano ya kugawana madara nchini Zimbabwe inazungumzia masuala ya kiuchumi.Masuala hayo yanahusu kuimarisha na kuukuza uchumi.Tangu mwaka wa 2000,wakati serikali ya Zimbabwe ilianza hatua za kuvamia mashamba ya wazungu, uchumi wake ulianza kuporomoka vibaya,thamani ya sarafu yake ikashuka na nchi hiyo ikawa moja wa nchi ambazo ni ngumu kuendesha biashara duniani.
Pande mbili husika na makubaliano ya kugawana madaraka, zilikubaliana kutoa kipaumbele kuimarisha tena uchumi wa Zimbabwe,kushughulikia mpango wa kuinua kilimo, kuunda barala la taifa la uchumi ambalo litajumulisha wajumbe kutoka sekta zote nchini na pia kukubali pendekezo la jumuiya ya SADC kuhusu uchumi wa nchi hiyo kutoka uchunguzi uliofanywa na sekreterieti ya SADC.
Vionmgozi kadhaa wa jumuiya ya SADC wamezungumzia haja ya kuwa na msaada wa Zimbabwe haraka iwezekanvyo. Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele katika juhudi hiyo ambapo rais wa zamani wa nchi hiyo Thabo Mbeki alianzisha mchakato wa mpango wa kilimo wa kipindi cha msimu wa kati ya mwaka wa 2008 na 2009.
Idara za hazina,kilimo na mashauri ya kigeni za Afrika kusini,zimekuwa zinashughulikia juhudi za kupata pembejeo kwa ajili ya Zimbabwe kabla ya kuanza msimu wa kilimo.
Ingawa wakulima wa Zimbabwe tayari wameanza kupokea mbegu za mahindi pamoja na mbolea kutokana na juhudi za mwanzo, alikini haijabainika wazi ikiwa utawala mpya wa Afrika kusini chini ya rais Kgalema Motlanthe,utaendeleza juhudi za Bw Mbeki kuelekea Zimbabwe.Motlanthe amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Umoja wa Ulaya ulikaribisha makubaliano ya kugawna madaraka lakini likaongeza kuwa linasubiri kuona jinsi Mugabe na Tsvangirai watakavyo tekeleza mapatano hayo kabala ya kuahidi msaada.Hata hivyo baadhi ya msaada wa fedha usiokuwa na msharti unaonokana umeanza kuingia.
Serikali ya Zimbabwe imetangaza kuwa imeweza kupata dola millioni 80 kwa ajili ya kununulia mahindi na mafuta.Pesa hizo zimetoka kwa African Export Import Bank Afreximbank, ambalo ni taasisi ya kifedha yenye lengo la kukuza na kupanua biashara barani Afrika.