1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

SADC: Uchaguzi Zimbabwe haujakidhi mahitaji ya katiba

25 Agosti 2023

Matokeo ya mapema ya majimbo katika uchaguzi wa Zimbabwe yanaonyesha ushindani wa karibu kati ya chama tawala ZANU-PF na upinzani mkuu.

Bango la wagombea wa muungano wa upinzani CCC mjini Gweru
Bango la wagombea wa muungano wa upinzani CCC mjini GweruPicha: Zinyange Auntony/AFP via Getty Images

Wachambuzi wanaeleza kuwa chama cha ZANU-PF chake Rais Emmerson Mnangagwa kinatarajiwa kudumisha utawala wake wa miaka 43 madarakani nchini humo.

Matokeo yaliyotangazwa hadi sasa na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe yanaonyesha chama cha ZANU-PF kimeshinda viti 43 vya ubunge huku muungano wa upinzani wa wananchi kwa ajili ya mabadiliko CCC ukishinda viti 37, kati ya maeneo bunge yote 210.

Soma pia: Kura zaendelea kujumuishwa Zimbabwe

Matokeo ya urais bado hayajatangazwa baada ya zoezi hilo kuanza siku ya Jumatano, na hata kuongezwa muda katika baadhi ya wadi kutokana na kucheleshwa kwa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80, anawania muhula mwengine katika wakati ambapo nchi hiyo ya kusini mwa Afrika inakabiliwa na mfumuko wa bei na ukosefu mkubwa wa ajira. Wazimbabwe wengi wanategemea fedha zinazotumwa kwao na jamaa, na familia zinazoishi nje ya nchi ili kujikimu kimaisha.

Mpinzani wake mkuu ni wakili na mchungaji Nelson Chamisa, mwenye umri wa miaka 45.

Nafasi ya Zimbabwe kutatua mzozo wake wa madeni na kupata mikopo kutoka benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF iko hatarini, baada ya taasisi hizo za fedha kuweka bayana kwamba, kufanyika uchaguzi huru na wa haki ni moja kati ya masharti waliyoyaweka ili kuiruhusu Zimbabwe kuomba mikopo.

Serikali pamoja na tume ya uchaguzi zimeahidi kufanyika kwa uchaguzi huru japo baadhi ya wachambuzi wametilia shaka kauli hizo na kueleza juu ya uwezekano mkubwa wa uchaguzi huo kufanyika katika mazingira ya kuegemea upande wa Mnangagwa hasa kwa kuzingatia historia ya chama chake kutumia taasisi za serikali kuchakachua matokeo ya uchaguzi.

SADC: Uchaguzi umefanyika kwa amani

Viongozi wa muungano wa upinzani wakiwasili mjini Gweru kwa mkutano wa kisiasaPicha: Zinyange Auntony/AFP/ Getty Images

Timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC imesema kuwa zoezi la upigaji kura limefanyika kwa amani japo kulikuwepo kwa visa kadhaa kama vile ucheleweshwaji wa kupiga kura, kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa, upendeleo wa vyombo vya habari vinavyoegemea upande wa serikali na kushindwa kwa tume ya uchaguzi kuwapa nafasi wagombea kukagua daftari la wapiga kura.

"Baadhi ya vipengele vya uchaguzi havikukidhi mahitaji ya katiba ya Zimbabwe, sheria ya uchaguzi, kanuni na miongozo ya SADC inayoongoza uchaguzi wa kidemokrasia,” Mkuu wa waangalizi wa SADC Nevers Mumba, amewaambia waandishi wa habari leo Ijumaa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la Reuters katika mji mkuu Harare, ni kuwa mapema leo asubuhi, polisi ilifunga barabara karibu na kituo kikuu cha kujumlisha kura, huku raia wakizuiwa na kuhojiwa.

Katibu wa fedha wa chama tawala ZANU-PF Patrick Chinamasa aliwaambia waandishi jana kuwa chama hicho kinaelekea kupata thuluthi mbili ya wawakilishi katika bunge la kitaifa.

Soma pia: Upinzani Zimbabwe wadai kuwepo "wizi wa kura" uchaguzi mkuu

Matokeo ya mapema leo yameonyesha kuwa ZANU-PF imepata ushindi mkubwa katika maeneo ya vijijini huku muungano pinzani CCC ukitamba katika maeneo ya mijini, kama tu ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.

Chama tawala kimepata pigo kubwa baada ya tume ya uchaguzi kutangaza leo kuwa waziri wa fedha Mthuli Ncube amepoteza kiti chake cha ubunge kwa mpinzani wa muungano wa CCC.

Maelfu ya wafuasi wa muungano wa upinzani mjini Gweru Picha: Zinyange Auntony/AFP/ Getty Images

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutolewa kabla ya muda wa mwisho uliowekwa wa siku tano.

Chinamasa amesema chama tawala kinaelekea kupata asilimia 60 hadi 65 za kura za urais na kupuzilia mbali madai ya Nelson Chamisa kwamba alikuwa anaongoza. Ametaja madai hayo kama "ndoto za mchana.”

Mnangagwa alichukua usukani wa kuiongoza Zimbabwe baada ya mapinduzi ya mwaka 2017 yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe na baadae kushinda uchaguzi uliozua utata mnamo mwaka 2018.