SADC yakutana kuhusu Zimbabwe.
25 Juni 2008Viongozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika wanakutana nchini Swaziland kujadilia mgogoro nchini Zimbabwe.
Huku viongozi hao wakikutana rais Robert Mugabe kwa upande wake amesema uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa licha ya kujiondoa kwa mpinzani wake Morgen Tsvangirai ambae anasemekana ameomba jeshi la kimataifa kuingilia kati ili kulinda wananchi dhidi ya wanamgambo wa Mugabe.
Mkutano wa mjini Mbabane, mji mkuu wa Swaziland, ambao ni wa dharura umeitishwa na jumuia ya kikanda ya SADC kutokana na hali ilivyo nchini Zimbabwe kwa sasa.
Taarifa iliotolewa na serikali ya Tanzania ilisema kuwa Viongozi wa Tanzania, Angola na Swaziland wanashiriki kama wanachama wa tume ya siasa,ulinzi na usalama ya SADC.
Taarifa za awali zilisema kuwa viongozi wengine walioalikwa ni mwenyekiti wa sasa wa SADC, rais Levy Mwanawasa wa Zambia, pamoja mpatanishi wa mzozo wa Zimbabwe kwa niaba ya SADC, rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Lakini msemaji wa rais Mbeki,Mukoni Ratshitanga, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Bw Mbeki hatahudhuria mkutano huo kutokana na kuwa hakupewa mwaliko.
Shinikizo dhidi ya Mugabe linazidi kupamba mpto .Baada ya mpinzani wake Tsvangirai kujiondoa katika mbio hizo mwishoni mwa juma kutokana na ghasia dhidi ya wafuasi wake na baadae kukimbilia ubalozi wa Uholanzi,baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani vitendo vya kinyama vinavyotendewa wafuasi wa upinzani.
Baraza la Usalama pia lilisema kuwa uchaguzi wa Ijumaa haufai kwani hautakuwa huru na wa haki.
Nae waziri wa mashauri ya kigeni wa Australia Stephen Smith aliliambia bunge serikali yake inaunga mkono kwa dhati wazo la kutofanyika uchaguzi huo wa ijumaa kani hauna tena maana yoyote.
Lakini Mugabe amepuuza lawama hizo pamoja na mapendekezo na kusema kuwa uchaguzi utaendelea mbele.
Mapema mpinzani wake aliokomafichoni katika ubalozi wa Uholanzi mjini Harare,Morgen Tsvangirai, alikuwa ameuhimiza Umoja wa Mataifa kumtenga rais Mugabe na kusema kikosi cha kulinda amani kinahitajika nchini Zimbabwe.
Kupitia makala aliyoandika na kuchapishwa na gazeti la Uingereza la The Guardian,Tsvangirai ameuomba Umoja wa Mataifa kulaani ghasia zinazoendelea nchini Zimbabwe.
Aidha amesema kuwa kunahitajika jeshi la kulinda amani ambalo ni la kulinda wananchi wala sio kukabiliana na vikosi vya dola.
Uchaguzi wa Ijumaa ulikuwa ni marudio kati yake na Mugabe Tsvangirai alishinda duru ya kwanza iliofanyika mwezi Machi,lakini takwim rasmi zilionyesha kuwa hakupata ushindi wa moja kwa moja hivyo ikabidi kura kupigwa tena ili kumpata mshindi.
Sasa uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa na Mugabe hatakuwa na mpinzani.
Na haijulikani mkutano wa kikanda wa SADC wa mjini Mbabane utaamua nini kuhusu suala hilo.