1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia na Eritrea zaanza safari ya mahusiano mema

18 Julai 2018

Ndege ya kwanza ya abiria kutoka Ethiopia kuelekea Eritrea imeondoka hii leo wakati njia za angani zikifunguliwa tena baina ya nchi hizo mbili baada ya kukubaliana kumaliza mgogoro uliodumu miaka 20.

Äthiopien Addis Abeba Ethiopian Airlines neuer Linienflug nach Eritrea
Picha: Getty Images/AFP/H. Tadese

Shirika la ndege la Ethiopia, liliweka picha ya ndege yake yenye nambari za safari ET0312 katika mtandao wake wa kijamii wa twitter, ikiondoka mjini Addis Ababa kuelekea mji Mkuu wa Eritrea Asmara.

Miongoni mwa waliokuwemo katika ndege hiyo ni watu waliokuwa na hamu ya kuungana na familia zao baada ya kutenganishwa na mgogoro huo wa muda mrefu. 

Aliekuwa waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn,  pia alikuwepo katika ndege hiyo.

Kulingana na mwandishi habari wa shirika la AFP aliyeabiri ndege hiyo, kinywaji aina ya champagne kilitolewa  kwa abiria wote waliogongeshana glasi muda mfupi baada ya ndege hiyo kuondoka.

Rubani wa shirika la ndege la Ethiopia Kapteni Yoseph Hailu Picha: Reuters/T. Negeri

Vile vile wahudumu wa ndege waliokuwa wakitabasamu waliwakabidhi abiria wote maua.

Shirika la ndege la Ethiopia moja ya mashirika ya ndege yanayokuwa kwa haraka barani Afrika limesema litakuwa na ndege moja kila siku ya kwenda na kurudi kutoka addis Ababa hadi Asmara nchini Eritrea.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo  Tewolde GebreMariam, ameongeza kuwa huenda wakaongeza safari hizo hadi mara mbili au mara tatu kwa siku kutokana na wingi wa abiria.

Mahusiano mapya ya Ethiopia na Eritrea yanatarajiwa kupiga jeki uchumi wa nchi hizo.

Siku ya Jumatatu rais wa Eritrea Isaias  Afwerki alifungua tena ubalozi wa Eritrea mjini Addis Ababa. Kurejesha mahusiano yaliovunjika kwa muda mrefu baina ya Ethiopia na Eritrea kunatarajiwa kupiga jeki uchumi wa nchi hizo mbili. Wakati huo huo shirika la Amnesty International limesema amani mpya iliyopatikana inapaswa kuwa nafasi mpya ya mabadiliko kwa Eritrea moja ya mataifa yaliotengwa duniani.

Wafanyakazi wa shirika la ndege la Ethiopia wakijitayarisha kabla ya kuanza safari ya kwanza kutoka Addis Ababa hadi Asmara, Eritrea.Picha: Reuters/T. Negeri

Juhudi za kidiplomasia za kuleta amani kati ya mataifa hayo mawili zilianza  mwezi uliopita wakati mpenda mabadiliko Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia Abiy Ahmed aliye na miaka 42, allipoukubali mpango wa amani uliomaliza vita vya mpakani vilivyoanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2000.

Baada ya hapo viongozi wa Ethiopia na Eritrea walianza mara moja kutembeleana na kukaribishana kwa kukumbatiana. Jamii ya Kimataifa kwa upande wake imakaribisha na kusifu kumalizika kwa moja ya migogoro ya muda mrefu barani Afrika.

Mawasiliano ya simu yamerejeshwa na mahusiano ya kiuchumi yameanza kurejeshwa huku Ethiopia nchi isiokuwa na bandari ikiwa na nia ya kujiendeleza kupitia bandari ya Eritrea ya eneo la bahari nyekundu.

Mwandishi: Amina Abubakar AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW