Saif Al Islam akamatwa Libya
20 Novemba 2011Luis Moreno Ocampo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama inayopambana na uhalifu wa kivita iliopo The Hague Uholanzi, inayokuwa inamsaka Saif kwa uhalifu dhidi ya binaadamu, amesema ataelekea nchini Libya katika wiki zinazokuja kujadili wapi na vipi Saif Al Islam atashtakiwa.
Hapo jana Saif alisafirishwa hadi katika mji uliokuwa ukidhibitiwa na waasi uliopo magharibi mwa Tripoli, Zintan, ambako waziri mkuu wa mpito Abdurrahim el Keib amesema sheria za kimataifa zitaheshimiwa.
Aliongeza hatahivyo kuwa watu wa Libya wanataka kesi dhidi ya Saif ifanyike nchini humo. Umoja wa Ulaya na shirika la kujihami NATO, zimetoa wito kwa viongozi wapya wa Libya wa kushirikiana na mahakama ya kimataifa.
Kanda za video za televisheni zilimuonyesha Saif akiwa na majeraha ya mkononi. Alikamatwa karibu na mji uliopo jangwani,Obari, akiwa na wapambe wake kadhaa waliokuwa na silaha.
Walibya wengi walimiminika katika barabra za nchihiyo walipopokea taarifa za kukamatwa kwa Saif.
Mwandishi Maryam Abdalla/rtre, dpae, ape
Mhariri:Mtullya Abdu