1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Saif al-Islam Gaddafi auawa

4 Februari 2026

Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ameuawa kupitia kile ofisi yake ilichosema ni "tendo la kihalifu na la woga" katika mji wa magharibi mwa nchi hiyo, Zintan.

Saif Al Islam Al Gaddafi
Saif al-Islam Gaddafi wakati wa uhai wake alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye serikali ya baba yake, Marehemu Muammar Gaddafi.Picha: Studiofacts Rights

Kwa mujibu wa wakili wake, Khaled al-Zaidi, Saif aliuawa na watu wanne waliokuwa wameficha sura zao walioivamia ofisi yake siku ya Jumanne (Februari 3).

Kituo cha televisheni cha al-Arabiya, kimeripoti kwamba Saif, aliyekuwa na umri wa miaka 53, aliuawa akiwa kwenye bustani ya nyumba yake huko Zintan, kikimnukuu mtu wa karibu na familia ya Gaddafi.

Kulikuwa na uvumi kwamba wanamgambo walio karibu na serikali yenye makao yake mjini Tripoli inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibeh wamehusika na mauaji hayo, ingawa wenyewe wamekanusha.

Saif al-Islam alikuwa anasemakana kupanga kurejea kwenye siasa, hatua iliyotazamwa kama kikwazo kwa Dbeibeh na washirika wake.

Hadi kifo chake, mtoto huyo wa Gaddafi alikuwa akitakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati wa machafuko ya Libya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW