Sakata la udukuzi: Marekani yaigeuka Ulaya
30 Oktoba 2013Wakuu hao wa mashirika ya ujasusi ya Marekani waliyakanusha kuwa ni uongo, madai kwamba mashirika yao yalinasa mawasiliano ya mamilioni ya simu, na kusema magazeti ya Ulaya yaliyochapisha madai hayo, hayakuelewa data walizokuwa wanazitumia kutoa madai hayo.
Maelezo hayo yamekuja wakati afisa wa juu wa Marekani akisema Rais Barack Obama alikuwa akitafakari kuwapiga marufuku majasusi wa Marekani kunasa mawasiliano ya ya simu za viongozi wa mataifa washirika, kufuatia hasira za Ujerumani juu ya madai kwamba mawasiliano ya Kansela Angela Merkel yalidukuliwa.
Mkuu wa NSA, Jenerali Keith Alexander, na mkuruguenzi wa usalama wa taifa, James Clapper, walitoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani na kusema kwamba msingi wa ripoti hizo ulikuwa kutolewa taarifa zilizokabidhiwa kwa magazeti ya Ulaya na Snowden.
"Madai ya waandishi wa habari wa gazeti la Le Monde la Ufaransa, El Mundo la Uhispania na L'Espresso la Italia kwamba NSA ilikusanya mamilioni ya taarifa za mawasiliano ya simu hazina ukweli wowote. Kwa kuweka mambo wazi kabisa, hizo siyo taarifa tulizozikusanya kuhusu raia wa Ulaya. Ni taarifa ambazo sisi pamoja na washirika wetu wa NATO tulizikusanya katika kuhakikisha usalama wa mataifa yetu na kusaidia operesheni zetu za kijeshi," alisema Jenerali.
Ufaransa, Uhispania zaumbuliwa
Masaa machache kabla ya hapo, jarida la Wall Street liliripoti kwamba uchunguzi wa kielektroniki ulifanywa na mashirika ya kijasusi ya Ufaransa na Uhispania nje ya mipaka ya mataifa yao, na wakati mwingine katika uwanja wa vita na kutoa taarifa zao kwa NSA.
Ikiwa madai hayo yatakuwa kweli, yanaweza kuzifedhehesha serikali za mataifa ya Ulaya, ambazo zimeipinga kwa nguvu Marekani kwa madai ya kuwafanyia ujasusi raia wake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya bunge la Marekani, Dianne Feinstein, aliunga mkono utetezi wa wakuu hao wa ujasusi na kusema kuwa Marekani haikuzichunguza Ufaransa na Ujerumani, bali nchi hizo ndizo zilikuwa zinakusanya taarifa hizo, na kwamba Marekani ilikuwa inakusanya tu taarifa katika maeneo ya kivita ya NATO kama vile Afghanistan.
Kuchunguzana ni mchezo wao
Hakukuwa na majibu ya mara moja kutoka kwa mashirika ya kijasusi ya mataifa ya Ulaya yaliyotajwa, lakini Alexanser na Clapper waliwambia wabunge kuwa mataifa ya kigeni pia yalikuwa yakiwafanyia ujasusi viongozi wa Marekani, na kufafanua kuwa kuwachunguza viongozi wa kigeni ndiyo msingi wa mchezo wa ujasusi kimataifa.
Wakati huo huo, maafisa wa ujasusi wa Ujerumani wanatarajiwa kukutana na wawakilishi wa mashirika ya ujasusi ya Marekani katika lkulu ya White House leo, kujadili madai ya ujasusi wa Marekani. Ujumbe wa Ujerumani unawahusisha mshauri wa sera ya kigeni wa Kansela Merkel na mratibu wa idara ya ujasusi ya Ujerumani.
Kwa upande wa Marekani, ujumbe wake unaowajumuisha mshauri mkuu wa usalama wa Rais Obama, Suzane Rice, mkurugenzi wa usalama wa taifa James Clapper na msaidizi wa rais wa usalama wa ndani na mapambano dhidi ya ugaidi, Lisa Monaco.
Rais Obama na Kansela Merkel walikubaliana katika mazungumzo mafupi kwa njia ya simu wiki iliyopita kuimarisha ushirikiano wa nchi zao katika masuala ya ujasusi, na msemaji wa NSA, Caitlin Hayden, alisema mkutano huu ni sehemu ya majadiliano hayo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae, afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo