Sala maalum kwa Khaemenei yafanyika Iran
10 Aprili 2026
Picha za televisheni ya taifa zilionyesha umati mkubwa ukihudhuria sala hiyo iliyoongozwa na imamu Mohammad‑Javad Haj Ali Akbari.
Sala hiyo ilifanyika katika kaburi la kiongozi wa mapinduzi Ruhollah Khomeini, aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, yaliyouondoa madarakani utawala wa Mohammed Rheza Palav,i hatua iliyoiingiza madarakani serikali ya Jamhuri ya kiislamu. Ruhollah Khomeini alizaliwa mwaka 1902 na kufariki dunia mwaka 1989.
Maombolezo ya Ayatollah Ali Khamenei yalianza siku ya Jumatano na kwenda sambamba na kumalizika kwa kipindi cha siku 40 cha maombolezo ya Khamenei yaliyokuwa yanafanywa na kwa waislamu wa dhehebu la shia. Khamenei aliuwawa Februari 28 katika mashambulizi ya mwanzo kabisa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Haijawa wazi hadi sasa ni lini hasa Khamenei atakapozikwa baada ya mauaji yake. Kiongozi huyo wa Iran aliyeiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma, anatarajiwa kuzikwa katika eneo alikozaliwa la Mashhad Kaskazini Mashariki mwa Iran.
Mwanawe wa kiume, Mojtaba Khamenei, bado hajaonekana hadharani tangu alipoteuliwa kuchukua rasmi cheo cha baba yake mnamo Machi 8 hatua inayoendelea kuzua wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya, jukumu lake na mahali aliko.
Pakistan yachukua jukumu la upatanishi
Haya yanajiri wakati Pakistanikichukua jukumu la kuwa mpatanishi kwa pande hasimu katika mgogoro huo ambao ni Marekani, Israel na Iran. Uamuzi wa Pakistan kuchukua jukumu hilo huenda ukawa uliwashangaza wengi lakini utakumbuka kuwa Pakistan ina mahusiano mazuri sana na Jamhuri hiyo ya kiislamu.
Iran ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza kuitambua Pakistan baada ya kujitangazia uhuru wake mwaka 1947 na amebakia kuwa jirani wa karibu wanaopakana upande wa kusini. Nchi zote mbili ni nchi za kiislamu japokuwa wengi wa waislamu walioko Pakistan ni wa dhehebu la Sunni na wa Iran ni wale wa kishia.
Kando na Iran, Pakistan pia ina mahusiano mazuri ya kidiplomasia na Marekani. Licha ya mvutano uliokuwepo kati ya nchi hizo mbili kufuatia Marekani kudai kuwa Pakistan inawahifadhi magaidi akiwemo Osama Bin Laden kiongozi wa Alqaeda aliyeuwawa na Marekani, Washington inaitazama nchi hiyo kama mshirika wake aliye nje ya Jumuiya ya Kujihami NATO
Kwa sasa Naibu rais wa Markani JD Vance ameelekea Pakistan kwa mzungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa Iran.