1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sall atangaza kuondoka madarakani Aprili 2

23 Februari 2024

Rais Macky Sall wa Senegal amesema atahitimisha muhula wake kama anavyotakiwa na katiba hapo mwezi wa Aprili 2, lakini amekwepa kutangaza tarehe rasmi ya uchaguzi wa urais kama anavyotakiwa na Mahakama ya Katiba.

Rais Macky Sall wa Senegal
Rais Macky Sall wa SenegalPicha: Sylvain Cherkaoui/AP/picture alliance

Akizugumza na waandishi wa habari siku ya Alhamis (Februari 22), Sall alisema kwa vyovyote iwavyo asingeliongeza muda wa kuwapo kwake madarakani ifikapo tarehe yake ya mwisho aliyopewa na katiba.

"Kwa kuwa niliapishwa kuingia madarakani tareje 2 Aprili 2019, tarehe 2 Aprili 2024 inahitimisha muhula kamili wa miaka mitano, na hivyo mwisho wa mamlaka yangu niliyokabidhiwa. Na nakusudia kukomea hapo hapo. Baada ya tarehe 2 Aprili, nadhamiria kuondoka madarakani kama rais wa jamhuri hii." Alisema kwenye mazungumzo hayo yaliyorushwa na televisheni ya taifa.

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi Senegal lazusha kizaazaa

01:33

This browser does not support the video element.

Soma zaidi: Marekani yataka uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa Senegal

Awali, Sall alikuwa ametangaza kuuahirisha uchaguzi kwa muda usiojulikana, uamuzi ambao baadaye uliridhiwa na bunge kwa kuweka kipindi cha miezi kumi, akisema kulikuwa bado na utata juu ya nani angeliweza kuwania uchaguzi huo. 

Mbali na kupingwa navyama vya upinzani, asasi za kiraia na maandamano mitaani, uamuzi huo baadaye ulipingwa pia na Mahakama ya Katiba ya Senegal, iliyotamka kwamba ulikuwa kinyume na sheria.

Mahakama ya Katiba iliiamuru serikali kutangaza haraka tarehe mpya ya uchaguzi, lakini hadi sasa serikali ya Sall haijafanya hivyo.

Mkutano na vyama vya kisiasa

Kwenye mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari, Sall hakuweka wazi ni lini angelitangaza uchaguzi mpya, ingawa alisema alikuwa anakusudia kukutana na viongozi wa kisiasa kujadiliana kuhusu hilo.

Maandamano ya kupinga kuahirishwa uchaguzi nchini Senegal.Picha: John Wessels/AFP

"Nchi hii haiwezi kukaa bila ya kuwa na rais wa jamhuri. Majadiliano yajayo bila shaka yataamua au kupendekeza hatua za kuchukuwa ili tusonge mbele. Natarajia itakuwa hivyo. Natarajia watu ambao watakutana nami watayazingatia maslahi ya taifa kwenye suala hili. Lakini nitasikiliza kitakachosemwa kwenye majadililiano hayo, na baadaye, Mahakama ya Katiba itaweza kuweka mambo sawa." Alisema.

Soma zaidi: Watu waandamana Senegal kupinga uamuzi wa Rais kuahirisha uchaguzi

Senegal imekuwa ikichukuliwa kama mojawapo ya mataifa yaliyofanikiwa kwa kuwa mfumo imara kwa kidemokrasia, lakini mzozo uliozuka kutokana na uamuzi wa Sall kuahirisha uchaguzi umesababisha machafuko ya kisiasa na hata vifo. 

Tangu Sall atowe uamuzi wake huo, ambao sasa anaonekana kuufuta kutokana na shinikizo la kisiasa na kisheria analokabiliana nalo, watu watatu wamekwishauawa na vyombo vya usalama wakiwa kwenye maandamano ya upinzani. Wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Upinzani umepanga maandamano mengine mwishoni mwa wiki hii, wakimtuhumu Sall kwa kujaribu kung'ang'ania madaraka.

Vyanzo: AP, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW