Samia: Maridhiano na umoja ni dira ya Tanzania 2026
1 Januari 2026
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameukaribisha mwaka 2026 kwa wito wa mshikamano wa kitaifa, maridhiano ya dhati na kuimarisha ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa taifa linahitaji uponyaji wa pamoja baada ya kipindi kigumu cha kisiasa na kijamii.
Akihutubia taifa kutoka Tunguu, Zanzibar, Rais Samia alisema serikali imeanza rasmi maandalizi ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa itakayohusisha wadau wote muhimu nchini.
"Tunapoanza mwaka 2026, serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kuanzisha Tume ya Maridhiano. Tutashirikisha wadau kukubaliana muundo wake, majukumu yake na namna ya utekelezaji wake,” alisema Rais.
Alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na haja ya kuimarisha umoja wa kitaifa baada ya mwaka uliotikisa mshikamano wa kijamii na kisiasa nchini.
Mwaka mgumu wa kisiasa na wito wa uvumilivu
Rais Samia alikiri kuwa kipindi kilichoelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kilikuwa kigumu kwa Watanzania wengi, kikishuhudia mvutano wa kisiasa na maandamano yaliyosababisha maafa makubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Katika mazingira hayo, aliwataka wananchi kuwa wavumilivu, wenye ukomavu wa kisiasa na uzalendo wa dhati.
"Tusikubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo zitugawe na kutupotezea malengo ya taifa,” alisema.
Rais pia aliwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha au wapendwa wao katika matukio mbalimbali ya mwaka uliopita.
"Tumeondokewa na wapendwa wetu, tunaendelea kuwaombea,” alisema kwa huzuni.
Uchumi waimarika licha ya changamoto
Akizungumzia hali ya uchumi, Rais Samia alisema Tanzania iliendelea kufanya vizuri licha ya changamoto za kimataifa na za ndani, huku uchumi ukikua kwa asilimia 5.8 mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 5.2 mwaka 2024.
Alibainisha kuwa mfumuko wa bei uliendelea kudhibitiwa kwa wastani wa asilimia 3.4, hali iliyosaidia kupunguza shinikizo la gharama za maisha kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Rais, akiba ya fedha za kigeni imeongezeka hadi kufikia dola bilioni 6.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa kwa zaidi ya miezi mitano, huku deni la Taifa likibaki kuwa himilivu.
"Serikali itaongeza umakini katika usimamizi wa fedha za umma na kuongeza mapato,” alisisitiza.
Maji Dar es Salaam na athari za tabianchi
Rais Samia alisema changamoto ya maji iliyojitokeza mwaka 2025, hasa jijini Dar es Salaam, ilisababishwa na vipindi virefu vya ukame kati ya Mei na Oktoba.
"Tulichukua hatua za haraka kutatua changamoto ya maji jijini Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha zitarejesha upatikanaji wa maji,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Kidunda na awamu ya pili ya Mradi wa Maji wa Kimbiji, kwa lengo la kumaliza kabisa tatizo la maji katika jiji hilo.
Rais pia alitoa pole kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko na upepo mkali uliokumba baadhi ya maeneo ya nchi mwishoni mwa mwaka, akizitaka taasisi husika kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na majanga.
Ajenda ya maendeleo na diplomasia ya uchumi
Rais Samia alithibitisha dhamira ya serikali ya kuendelea kutekeleza ajenda ya maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala, akisema taarifa ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 itatolewa kwa umma mwezi Februari 2026.
Aidha, alisema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi, ili kuvutia uwekezaji, kupanua biashara na kukuza ustawi wa wananchi.
"Tanzania inaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda,” alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwahimiza Watanzania kuukaribisha mwaka 2026 kwa mshikamano, nidhamu na dhamira ya pamoja ya kulijenga taifa.
"Umoja wa kitaifa ni ajenda yetu kuu tunapouanza mwaka 2026,” alisema, akisisitiza kuwa amani na maendeleo ya taifa vitapatikana tu endapo Watanzania watasimama pamoja licha ya tofauti zao.