1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia aitaka Polisi kusimamia maadili, awakosoa mabalozi

17 Septemba 2024

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amelitaka jeshi la polisi nchini humo kuendelea kusimamia maadili ya askari, akisema halipaswi kuhusika au kuhisishwa katika ukiukaji wa haki za sheria wanazozisimamia.

Tanaania |Maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi la polisi
Rais Samia akikagua gwaride la polisi katika maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo.Picha: Florence Majani

Rais Samia Suluhu Hassan, ameyasema hayo katika hafla ya kufunga mkutano mkuu wa maafisa waandamizi wa jeshi la polisi kwa mwaka 2024, na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi la Polisi Tanzania.

Akizungumza  mara baada ya kukagua gwaride na kupitia maonyesho mbalimbali yaliyoandaliwa na jeshi hilo katika mkutano huo Rais Samia, alitumia fursa hiyo, kulitaka jeshi la polisi, kusimamia maadili ili kuepuka kuhusika au kuhisiwa katika ukiukwaji wa sheria wanaozisimamia.

"Tumevumiliana kwenye mengi lakini kwenye kulinda tunu na amani ya nchi hii, nirudie tena, sitakuwa na muhali kwa yeyote, anayeratibu, anayershiriki, hata anayetekeleza mipango hii miovu," alisema Samia.

Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja wakati taifa likiwa katika taharuki ya matukio ya mauaji na utekaji wa raia wakiwamo makada wa chama kikuu cha upinzani nchini Chadema.

Miongoni mwa matukio yaliyozua taharuki ni pamoja na lile lililohusisha kutekwa na kuuwawa Ali Kibao, Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, na  mwili wake kutupwa katika msitu wa Ununio, Tegeta jijini Daresalam, tukio ambalo licha ya kuzua hofu, liliwaibua pia wanaharakati, wanasiasa na wanadiplomasia kukemea mfululizo wa matukio hayo nchini.

Polisi wa kike akionyesha ukakamavu mbele ya rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhmisho ya miaka 60 ya jeshi la polisi la Tanzania.Picha: Florence Majani

Awataka mabalozi waache kuingilia yasiowahusu
 

Katika hafla hiyo Rais Samia amejibu tamko lililotolewa na mabalozi wa mataifa kadhaa waliotaka uchunguzi wa haraka kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yalizusha taharuki katika siku siku za hivi karibuni, akisema Tanzania ni nchi huru na haipaswi kuelezwa cha kufanya kwenye mambo yake ya ndani.

Rais Samia amesema haamini kama mabalozi hao walichokitamka ni maagizo ya wakuu wao wa mataifa, na kuahidi kuwachongea kwa mamlaka zao za uteuzi.

Soma pia:Polisi ya nchini Tanzania imeyazuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa Septemba 23 

Mabalozi wa mataifa 15 mengi yao yakiwa ya Umoja wa Ulaya, walitoa tamko wakitaka kuharakisha uchunguzi wa matukio ya utekaji nyara na mauaji, kufuatia kutekwa na kisha kuuawa kikatili kwa kada wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, Chadema. 

Mabalozi waliotoa tamko hilo ni pamoja na wa Uingereza, Ubelgiji, Canada, Denmark, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Ireland, Italia, Poland, Uhispani, Sweden na Uswisi, huku Marekani ikitoa tamko la pekee juu ya matukio hayo.

Katika tamko lao mabalozi hao walikaribisha wito wa rais wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu matukio ya utekaji na mauaji, na kutaka wapinzani walindwe ili kufanikisha falsafa ya 4R ya rais Samia, ambayo inawakilisha maridhiano (Reconciliation), ustahamilivu (Resilience), mabadiliko (Reforms) na kujenga upya (Rebuilding).

Mauaji ya kada wa Chadema Ali Mohamed Kibao na watu waliomchukua kwenye basi baada ya kujitambulisha kuwa askari wa usalama, yameongeza mbinyo kwa serikali kushughulikia kitisho hicho.Picha: Chadema

Hata hivyo Samia amesema falsafa yake ya R4 si kigezo cha wapinzani kutumia uhuru huo vibaya  na akalitaka jeshi la polisi kusimamia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani 2025.

Soma pia: Viongozi wa upinzani Tanzania waachiwa wakati polisi ikionya juu ya uvunjifu wa amani

"Ukimya wangu sio ujinga, na wala kuzungumza sana si werevu, kuzungumza sana ni udebe tupu haliachi kuvuma," alisema kiongozi huyo. Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania wamesema ni wajibu wa Samia kama kiongozi mkuu wa taifa kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wote.

"Huu mnyororo wa matukio ya watu wasiojulikana, yanapaswa kuchukuliwa kwa umakini zaidi na Rais Samia kuliko mtu mwingine yeyote kwa sababu  yeye ndiye mlinzi mkuu wa maisha ya watanzania na ni yeye ndiye mlinzi mkuu wa katiba," alisema Lugman Maloto, Mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi.

Alitaka jeshi la polisi kukumbatia teknolojia

Kiongozi huyo wa Tanzania alilitaka pia jeshi la polisi, kujipanga kiteknolojia ili kudhibiti uhalifu wa mtandaoni hasa taarifa za uzushi na uongo, alinukuu takwimu za ofisi ya taifa ya takwimu akisema, uhalifu wa mitandaoni umeongezeka kwa asilimia 36.1 kutoka matukio 1006  mwaka 2022, hadi matukio 1366 Desemba mwaka jana.

Chadema kuwasilisha mashtaka dhidi ya Kamishna wa Polisi Tanzania

02:46

This browser does not support the video element.

Katika hafla hiyo, Rais Samia pia alikagua gwaride na maonyesho mbalimbali ya jeshi la polisi, kisha akawapa tuzo, askari 10, walioingia jeshini kabla na muda mfupi baada ya uhuru, wakiwamo wanawake wanane wa kwanza kujiunga na jeshi hilo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW