Uganda, Tanzania zaidhinisha ujenzi wa bomba la mafuta
20 Mei 2021Mkataba huo uliotiwa saini Alhamisi katika ikulu jijini Dar es Salaam, ni hatua ya mwisho ambayo inawezesha sasa ujenzi wake kuanza mara moja na kwamba makampuni mawili makubwa ya Total ya Ufaransa na Sinoc ya China yanagharimia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,443 kwa kushirikiana na mashirika yanayohusika uzalishaji mafuta ya Tanzania na Uganda.
Utiaji saini kama huu ulifanyika pia Uganda Aprili 11, na kushuhudiwa na marais wa pande zote mbili huku kampuni zitakazoshiriki katika ujenzi wake zikiwa wahusika wakuu.
Inakadiriwa kwamba ujenzi wa bomba hilo litakaloanzia Hoima, Uganda na kisha kupita katika mikoa minane ya Tanzania hadi bandari ya Tanga utakamilika ifikapo mwaka 2024.
Kiasi cha shilingi bilioni 28 kimeshatengwa kwa ajili ya ulipaji wa fidia katika maeneo ambayo bomba hilo la usafirishaji wa mafuta ghafi litapita.
Soma pia: Uganda na Tanzania zasaini mkataba ujenzi wa bomba la mafuta
Waziri wa Nishati wa Tanzania, Medard Kalemani amesema serikali zote mbili zinatarajiwa kufaidika kwa sehemu kubwa kutokana na ujenzi wa bomba hilo kwa kuwa na umiliki wa asilimia 15 kwa kila upande.
Kuhusu mgawanyo wa mapato yatokanayo ya mradi huo, Tanzania inatarajia kupata gawio la asilimia 60, wakati asilimia iliyosalia 40 ikichukuliwa na Uganda.
Mgawanyo wa mapato yatokanayo na mradi
Kutokana na sehemu kubwa ya bomba hilo kuwa sehemu ya Tanzania, taifa hili linatarajia kuzalisha ajira zaidi ya asilimia 60 huku likitarajia pia kuwavutia wawekezaji wengi pindi usafirishaji wa mafuta hayo utakaanza.
Wakizungumza kwenye hafla hiyo, marais wote wawili walitaka kutokuwepo tena kwa visingizio vitakavyochelewesha mradi huo ambao majadiliano yake yalianza tangu miaka mitano iliyopita.
Soma pia: Kenya na Tanzania zatia mikataba ya kibiashara na uwekezaji
Mbali na hilo, Rais Museveni alihoji kiu ya wananchi kudai maendeleo kwa kuibana serikali wakati maendeleo kama hayo yanaweza kupatikana iwapo watazitumia fursa kama hizo zinazopatikana.
Kwa upande wake, Rais Samia alisema hana shaka mradi huo utakamilika na hivyo kufungua ukurasa mpya wa uchumi wa mafuta kwa nchi za Afrika.
Iwapo yale yaliyoandikwa kwenye makubaliano ya mradi huo yatatekelezwa kama ilivyoahidiwa, shughuli ya usafirishaji mafuta ng'ambo huenda ikaanza mwaka 2025.