Samia: Waliofuata mkumbo wafutiwe makosa
14 Novemba 2025
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuundwa kwa kamati maalum itakayochunguza mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliomrejesha madarakani, hatua inayolenga kuweka wazi ukweli wa kilichojiri katika siku za machafuko.
Akizungumza siku ya Ijumaa mbele ya Bunge katika hotuba yake ya kwanza na ambayo inalizindua bunge la 13 baada ya kuchaguliwa tena, Rais Samia amesema serikali haiwezi kupuuza vifo hivyo na kwamba familia zilizopoteza wapendwa wao zinastahili majibu.
"Nimesikitishwa sana na tukio hilo. Nazipa pole familia zote zilizopoteza wapendwa wao,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliibuka mshindi baada ya kupata asilimia 98 ya kura katika uchaguzi wa Oktoba 29, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Hata hivyo, matokeo hayo yalizua madai ya udanganyifu, huku ukandamizaji wa maandamano ukisababisha machafuko yaliyoendelea kwa siku kadhaa.
Mashirika ya haki za binadamu na vyama vya upinzani katika taifa hilo la Afrika Mashariki yanadai mamia ya wananchi waliuawa na vyombo vya usalama huku mtandao wa intaneti ukiwa umezimwa nchini kote.
Rais atangaza msamaha kwa watuhumiwa wa uhaini
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alitoa wito kwa vyombo vya dola kuwa na moyo wa huruma kwa waandamamanaji vijana ambao tu walifuata mkumbo na kuandamana, baada ya mamia yao kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini; kosa ambalo adhabhu yake ni hukumu ya kifo.
"Ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa hawakujua wanachokifanya. Kama mama wa taifa hili, nazielekeza taasisi za utekelezaji wa sheria kuangalia upya kiwango cha makosa yao,” alisema kiongozi huyo wa Tanzania.
Amesema wale waliokamatwa kwa kufuata mkumbo bila nia ya kutenda uhalifu wanapaswa kupewa nafasi ya kujirekebisha, akiitaka Ofisi ya Mkuu wa Polisi na taasisi nyingine kusimamia hilo kwa haki.
Hatua hii ya kuunda kamati ya uchunguzi inatarajiwa kupunguza hali ya sintofahamu na kujenga imani kwa umma, huku taifa likisubiri kwa hamu kile kitakachobainishwa katika uchunguzi huo.