San Suu Kyi akutana na viongozi wa upinzani baada ya miaka mitatu
9 Novemba 2007Kwa mujibu wa walioshuhudia, Aung San Suu Kyi alisafirishwa kutoka nyumbani kwake kutumia gari lenye vioo ambavyo mtu hawezi kuona ndani, hadi kwenye jumba moja la wageni la serikali, ambako mkutano ulipangwa kufanyika. Inasemekana hatua hiyo ya serikali ililenga kuzuia aibu.
Mwanadiplomasia kutoka Asia ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema Aung San Suu Kyi amekutana na mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung Kyi, aliyeteuliwa kuwa waziri wa mahusiano wa serikali ya kijeshi ya Myanmar mwezi uliopita, wakati ulimwengu mzima ulipokasirishwa na ukandamizaji wa maandamano ya kupigania demokrasia yaliyoongozwa na watawa wa kibuda mjini Yangon.
Muda mfupi baada ya mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, viongozi wa upinzani wa chama chake Aung San Suu Kyi walifika katika ukumbi wa mkutano huo. Msemaji wa chama cha Aung San Suu Kyi, National League for Democracy, Nyan Win, amesema mkutano umekuwa mzuri lakini hakutoa maelezo zaidi.
Katika hatua ya kushangaza majenerali wa jeshi la Myanmar walitangaza jana kwamba Aung San Suu Kyi angeruhusiwa kukutana na viongozi wa chama chake cha National League for Democracy.
Tangazo hilo lilitolewa saa chache baada ya mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa katika mzozo ya Myanmar, Ibrahim Gambari, kukamilisha ziara yake ya siku sita nchini humo. Lengo la ziara ya kiongozi huyo lilikuwa kujaribu kuushawishi utawala wa kijeshi wa Myanmar ukubali kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani wanaopigania demokrasia nchini humo.
Bwana Gambari amesema juhudi zinaendelea hivi sasa ambazo zitasaidia kuwepo mazungumzo kati ya viongozi wa upinzani na utawala wa kijeshi.
´Sasa kuna mchakato unaoendelea ambao unatakiwa kusaidia kuwepo mazungumzo ya maana kati ya serikali ya Myanmar na kiongozi wa upinzani, Aun San Suu Kyi.´
Ibrahim Gambari alikutana jana na Aung San Suu Kyi kwa muda wa saa moja na kutoa taarifa kwa niaba yake kabla kuondoka nchini humo. Katika taarifa hiyo alisema Aung San Suu Kyi yuko tayari kushirikiana na utawala wa kijeshi kuanza mazungumzo kuhusu hali ya baadaye ya Myanmar.
Mkutano wa leo kati ya Aung San Suu Kyi, afisa wa utawala wa kijeshi wa Myanmar na viongozi wa upinzani, umeelezwa kuwa ishara ya matumaini makubwa nchini Myanmar huku kukiwa na dalili kwamba utawala huo wa kijeshi huenda ukaanza mazungumzo kuhusu mageuzi ya kisiasa kwa kushirikiana na kiongozi wa upinzani, Aung San Suu Kyi.