1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanaa ilivyochangia uhuru wa Kenya

11 Desemba 2013

Si wanasiasa na wapiganaji wa Mau Mau pekee waliochangia kwenye uhuru wa Kenya, bali pia kuna wanafasihi na wasanii wengine waliotumia vipaji vyao vya muziki, maigizo, na lugha.

Mwanafasihi na mwandishi Ngugi wa Thiong'o wa Kenya.
Mwanafasihi na mwandishi Ngugi wa Thiong'o wa Kenya.Picha: picture-alliance/dpa

Mapambano ya kudai uhuru wa Kenya yalianza tarehe 20 Oktoba 1952 hadi 12 Desemba 1963, siku ambayo Kenya ilijikomboa kutoka kwenye mikono ya wakoloni kwa kupeperusha bendera yake yenyewe.

Kufikia siku hiyo, hata hivyo, mengi yalifanywa na wasanii mbalimbali wa nchi hiyo kuhakikisha mafanikio yake. Sanaa ya muziki, kwa mfano, ilikuwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano, ambapo wasanii walitoa nyimbo kadhaa zenye lengo la kuhamasisha vita dhidi ya wakoloni na kuujulisha umma umuhimu wa kujikomboa.

"Watu wengi sana waliimba nyimbo ambazo zinaweza kumfanya mtu ajue hii nchi ni yetu na lazima ikombolewe kutoka kwenye mikono ile ya wakoloni. Mimi ni mmoja wa wale waliokuwa kwenye bendi ya Kilimambogo ambao tulikuwa tumeimba nyimbo nyingi sana za nchi hii yetu ya Kenya." Anasema Aziz Abdi, mmoja wa wanamuziki wa Kenya walioshiriki katika juhudi hizo.

Lugha ya Kiswahili ambayo asili yake ni upwa wa Afrika ya Mashariki unaujumuisha pia baadhi ya maeneo ya pwani ya Kenya ya sasa, ilikuwa na mchango mkubwa sana katika mapambano ya uhuru wa Kenya.

Hugholin Kimaro ni mhariri na mwandishi wa gazeti la Taifa Leo, moja kati ya magazeti machache yanayotumia lugha ya kiswahili nchini humo, na ambaye pia alitumia sanaa ya uandishi katika mawasiliano wakati wa kupigania uhuru.

"Mzungu alipotutawala alitulemaza kwa kufikiria kwamba chochote kile kilichokuwa chetu sisi Waafrika kilikuwa ni ovyo kitu ambacho hakina maana. Wakati wa kupigania uhuru ilikuwa rahisi kwa watu kukitumia Kiswahili kuondoa tofauti zao za kikabila na kuweza kuwasiliana na kuweza kupashana habari kwa urahisi. Kilitumika kuwaunganisha, kikaondoa zile tofauti za kikabila, Mduruma kutoka kule Pwani akaweza kuwasiliana na Mkikuyu kutoka mkoa wa Kati, wakaweza kuwasiliana na Mluya kutoka mkoa wa Magharibi. Lakini fahari ya kuzungumza kiswahili ni kwamba ni lugha yetu pia."

Je, bado wasanii wanakumbukwa?

Wasanii wa kundi la muziki wa kizazi kipya la Camp Mulla la Kenya.Picha: Camp Mulla

Miaka 50 tangu Kenya ijitawale yenyewe kutoka ukoloni wa Waingereza ni kipindi cha kujivunia kwa Wakenya wote kwani kuna mengi yaliyofikiwa. Hata hivyo linapokuja suala la wasanii, bado suali linaloulizwa ni ikiwa wanathaminiwa kwa mchango wao.

Irene Kariuki ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kukusanya Mapato ya Wasanii nchini Kenya, na anasema nchi hiyo imekuwa ikitumia njia kadhaa kuwaenzi wasanii wake kutokana na mchango wao kwa jamii.

"Kuna wakati ambapo tunakuwa tunaandaa matamasha ya kuwatunuku vitu mbalimbali kutokana na kazi zao, kama vile fedha na zawadi. Huwa tunayaangazia maisha yao tangu walipoanza utunzi na uimbaji na wamechangia vipi katika nchi yetu ya Kenya." Anasema Bi Irene.

Hata hivyo, kauli ya Bi Irene haiendani na kile kinachosemwa na wasanii wenyewe, kwani wanaona kuwa mchango wao mkubwa wakati wa kupigania uhuru umesahauliwa na serikali na jamii kwa ujumla.

Tuzo kwa wasanii wa Kenya

Kwa mfano, David Amunga ni mwanamuziki mkongwe na ambaye anasema licha ya muziki wake kusaidia sana kuunganisha na kuyapeleka mbele matwaka ya wanasiasa kwa kupigania uhuru wakati huo, bado hathaminiwi.

"Nakumbuka nyimbo kama zile tuliimba 'From America to Africa' tulikuwa tukihimiza ya kwamba Waafrika waliokuwa wakipelekwa Ulaya kujifunza elimu ya huko na kurudi hapa Kenya, warudi hapa Kenya wasaidie katika kujenga taifa jipya. Lakini nikiangalia katika maisha yangu sijapata kitu isipokuwa ile heshima nilipewa na rais ya OGW, sijapata kitu kingine na wengi walikufa wakiwa maskini." Anasema David.

Wakati Kenya ikiwa kwenye shamrashamra za miaka 50 tangu kupata uhuru wake, kama taifa linalojali basi linapaswa kukumbuka kuwa kuna wengi waliosaidia juhudi za kufanikisha uhuru huo. Si siri kwamba sanaa imeleta mchango mkubwa kama unavyojielezea wenyewe, lakini wasanii wanasahauliwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa ya Kenya, Agan Odero, anasema kwamba serikali ina mipango kabambe ya kuwaenzi wanamuziki akina David, ambao mchango wao kwa vyovyote ni mkubwa sana kwa sio tu harakati za uhuru, bali pia kwa ujenzi mpya wa Kenya baada ya uhuru huo.

"Kutakuwa na zile nyimbo ambazo watu wametambua zilivuma sana kati ya wale Wakenya wanamuziki ambao walikuwepo kuanzia ile miaka 10 ya kwanza ya uhuru, miaka 10 ya pili hadi sasa miaka 50. Kwa hiyo, kwa kila miaka 10 kutakuwa na santuri maalum ambayo itatengenezwa na pale kutakuwa tuseme na nyimbo kama 10 ama 12 ambazo watu wamechagua wakasema katika hizo enzi, hizo kweli zilisifika Kenya nzima na watu wanatambua mpaka wa leo, wapewe tuzo ya kitaifa." Ndivyo asemavyo Odero.

Mwandishi: Flora Nzema
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi