1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sanaa

Sanaa na umuhimu wa kuleta matumaini

Bryson Bichwa
14 Aprili 2025

Kazi ya sanaa ina nguvu kubwa sana katika jamii ikiwa itatumika vizuri. Hata kwenye maeneo yanayokumbwa na vita, sanaa imekuwa ikileta matumaini.

Gloria Shukrani, msanii wa Kongo aliyehamishia shughuli zake Afrika Kusini
Gloria Shukrani, msanii wa Kongo aliyehamishia shughuli zake Afrika KusiniPicha: Bryson Bichwa/DW

Gloria Shukrani ni msanii aliyekimbia vita vya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Leo hii, Gloria sio tu mkimbizi, bali ni msanii anayepaza sauti ya wanawake, watoto na wakimbizi kupitia maigizo na uimbaji. Katika jiji la Pretoria, Afrika Kusini, ndipo anapopaita nyumbani kwa sasa.

Gloria, ambaye ni msanii wa nyimbo za amani, uhamasishaji, usawa wa kijinsia, elimu na usawa katika jamii, anasema yeye ni simulizi ya mwanamke ambaye licha ya machungu ya vita, ameibuka kuwa mwangaza kwa wengine. "Nakumbuka nilivyowasili hapa kwa mara ya kwanza, sikuwa na kitu. Nilikuwa na matumaini tu. Lakini sanaa ilikua kama tiba kwangu," alifafanua Gloria.

Alianza uimbaji akiwa binti mdogo

Gloria alianza kuimba kanisani akiwa msichana mdogo mwenye umri wa miaka minane akiwa huko Uvira, Kivu Kusini. Akiwa na matumaini ya maisha bora, alilazimika kuelekea Afrika Kusini kutafuta hifadhi. Anasema safari yake haikuwa rahisi. Alikumbana na unyanyapaa, lugha ngeni, na utamaduni tofauti kabisa.

Kulingana na Gloria, wakati mwingine watu wanamuangalia kama sio mtu wa eneo anapoishi. ''Unasikia maneno kama 'rudi nyumbani kwenu', lakini kwa sasa hapa ndiyo nina amani. Na kupitia sanaa, najaribu kuwaeleza kuwa sisi sote ni binadamu," alibainisha msaani huyo. Katika kazi yake, Gloria anaimba nyimbo kuhusu wanawake wa Kiafrika, pamoja na maisha ya wakimbizi. Kila tungo kwake ina simulizi, si tu kuhusu maisha yake, bali ya wanawake wengi wakimbizi na watoto.

Gloria Shukrani akiwa na Bryson Bichwa Picha: Bryson Bichwa/DW

Lakini pamoja na kazi yake kuvutia, changamoto bado zipo. Kutafuta soko la kazi kama mgeni, pamoja na masharti ya ukaazi, ni kikwazo kingine. Anasema mara nyingi anajiunga na vikundi vya wanawake kutoka mataifa tofauti vilivyoko Pretoria, na wanabadilishana uzoefu wa mila zao, wanaimba, na kushirikishana simulizi, kwani kwa kufanya hivyo ndiyo namna ya kujenga daraja kati yao.

Gloria anasema kuwa sanaa yake ni silaha ya kupambana na ubaguzi na kutengeneza mshikamano. "Sanaa inanipa nafasi ya kuzungumza bila kuogopa. Hata kama lugha ni tofauti, lakini ujumbe ulioko kwenye nyimbo zangu za Kiingereza unawafikia," alisisitiza Gloria.

Sauti ya wasio na sauti

Gloria sio tu msanii, bali pia ni sauti ya wale wasiopata nafasi ya kusikika. Kupitia nyimbo zake, utunzi wake, maigizo na ushirikiano na wanawake kutoka mataifa mbalimbali, anaziunganisha jamii kwa utamaduni, huruma na mshikamano.

Katika dunia ambayo mara nyingi mipaka huwatenganisha watu, sanaa yake huwaleta watu pamoja. Ni ukumbusho kwamba kila mkimbizi ana simulizi, na kwa Gloria Shukrani, simulizi ilianza kwa machungu, lakini inaendelea kuwa na matumaini, ujasiri na hamasa ya kuleta mabadiliko katika jamii.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW