1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanchez yuko tayari kuchafua makubaliano ya Brexit

Yusra Buwayhid
24 Novemba 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya Jumapili watasaini makubaliano yanayojulikana kama Brexit ya Uingereza kujitoa katika umoja huo. Lakini Uhispania inadai mkataba wa maandishi kutoka Uingereza juu ya suala la Gibraltar.

Gibraltar
Picha: Regierung von Gibraltar

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, atakutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussesls, Ubelgiji Jumamosi kwa mazungumzo ya dakika za mwisho kuelekea mkutano wa kilele wa umoja huo utakaofanyika Jumapili. Mkutano huo utajadili mkataba wa Brexit wa Uingereza kujitoa katika muungano huo . May atakutana na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, pamoja na Rais wa Baraza la umoja huo Donald Tusk.

May anatarajia kuondoka mjini Brussels Jumapili akiwa na makubaliano thabiti kuhusiana na masharti ya kujiondoa kwa Uingereza kutoka katika Umoja wa Ulaya mnamo Machi 29, pamoja na makubaliano ya maandishi juu ya jinsi uhuasiano wa baadae utakavyokuwa kati ya pande hizo mbili, pale zitakapokubaliana juu ya mkataba wa kibiashara.

Mzozo wa eneo la Gibraltar - ambalo limekuwa likimilikiwa na Uingereza tangu mwaka 1713 huku Uhispania ikiwa bado inalipigania - ndio pekee uliobakia bila ya kupatiwa suluhu kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele wa Jumapili wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro sanchezPicha: picture-alliance/Gtresonline

Sanchez yuko tayari kuchafua makubaliano ya Brexit

Uhispani imepania kuyapinga makubaliano ya Brexit, huku ikitishia kuuzorotesha mkutano wa kilele wa Jumapili iwapo haitopatiwa uhakikisho wa kuwa na usemi juu ya mustakbali wa Gibraltar.

Huku mazungumzo yakiwa yanaendelea kati ya maafisa wa Uhispani, Uingereza na Umoja wa Ulaya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema iwapo hatopata anachokitaka yuko tayari kumharibia May mipango yake ya kuwataka viongozi wa Umoja wa Ulaya kusaini ahadi za kuwa na uhusiano wa karibu na Uingereza baada ya nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya mwezi Machi.

Wanadiplomasia mjini Brussels pamoja na wawakilishi wa serikali nyingine za mataifa ya Ulaya wamesema hawaamini kwamba Uhispania kweli itachafua mkutano wa kilele uliopangwa kwa umakini, ambapo May na viongozi wenzake wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya watakutana kwa masaa kadhaa Jumapili asubuhi. Lakini pia wamesema wamesikia maneno makali kutoka kwa mawaziri wa Uhispania, ambayo yameashtua na hawawezi kuyapuuza kabla ya kufanya mazungumzo na Sanchez.

Sehemu iliopo Gibraltar katika ramani

Wakati akiwa ziarani nchini Cuba, Sanchez amesema bado anangoja kuhakikishiwa kwamba katika siku za mbele hakutafanywa maamuzi yoyote yale kuhusu Gibraltar, kabla ya Uingereza na Uhispani kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja.

"Uhakikisho bado hautoshi na Uhispani itaendelea kuyapinga makubaliano ya Brexit. Kama kutapatikana makubaliano basi yatabatilishwa," amesema Sanchez hapo Ijumaa.

Wasiwasi wa EU kusambaratika kwa Brexit

Uhispania inatarajia kuungwa mkono na washirika wake wa Ulaya juu ya suala hilo ambalo chimbuko lake ni madai ya zaidi ya miaka 300 ya kutaka uhuru wa Gibraltar, kisiwa ambacho kipo karibuni na nchi hiyo licha ya kumilikiwa na Uingereza. Uingereza imeweka kambi yake ya jeshi la majini katika kisiwa hicho cha Gibraltar kilicho na wakaazi 30,000, huku kukiwa na masuali mengi juu ya uchumi wa eneo hilo baada ya kukamilika kwa mchakato wa Brexit.

Lakini madai ya Uhispani ya kutaka makubaliano yaliyoafikiwa hivi karibuni kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya yafanyiwe marekebisho ili nchi hiyo iwe na usemi zaidi juu ya suala la Gibraltar, huenda yakapingwa na Uingerza pamoja na washirika wake wa Umoja wa Ulaya, ambao wana wasiwasi juhudi zao za muda mrefu za kufikia makubaliano hayo huenda zikasambaratika.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW/rtre/ap

Mhariri: Sylvia Mwehozi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW