Sanders atangaza ushindi New Hampshire; Biden aanguka tena
12 Februari 2020Bernie Sanders , ambaye ni Seneta wa chama cha Democratic , ametokea wa kwanza akiwa na kiasi ya asilimia 26 ya kura, akifuatiwa na Pete Buttigieg, ambaye amepata kiasi ya asilimia 24, wakati ambapo zaidi ya asilimia 90 ya kura zimehesabiwa, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani ikiwa ni pamoja na CNN. Katika hotuba yake ya ushindi kwa wafuasi wake Bernie Sanders amesema huu ni mwanzo wa mwisho wa Donald Trump.
"Sababu ambayo imetufanya tushinde leo hapa New Hampshire, tumeshinda wiki iliyopita Iowa, kwa sababu ya kazi kubwa iliyofanywa na watu wa kujitolea. Na nataka kuwaambia leo, kwamba ushindi huu hapa ndio mwanzo wa mwisho wa Donald Trump."
"Haijalishi nani anashinda, na kwa hakika tunatumai itakuwa sisi, tutakuwa pamoja na kumshinda rais hatari kabisa katika historia ya hivi sasa katika nchi hii," sanders alisema. Wagombea wamekuwa wakitoa ujumbe wa umoja katika chama. Katika nafasi ya tatu bila kutarajiwa alikuwa Amy Klobuchar , akiwa na karibu asilimia 20 ya kura, ambaye anajaribu kuelekea katika nafasi ya juu kwa ujumbe ambao si rahisi lakini wenye matumaini. Elizabeth Warren na aliyekuwa makamu wa rais Joe Biden wametupwa nyuma wakiwa na asilimia 9 na 8 ya kura.
Mbio hizo za kuwania kuteuliwa sasa zinaelekea katika jimbo la Nevada na South Carolina, majimbo ambayo yana wakaazi zaidi wa Kilatino na Wamarekani wenye asili ya Afrika, tofauti na jimbo lenye wazungu wengi la New Hampshire.
Uchaguzi katika eneo la kaskazini mashariki , uchaguzi halisi wa kwanza wa mchujo katika mzunguko huo , unafuatia mjadala jimboni Iowa katika eneo la kati magharibi, ambako matokeo ya kura za mchujo yalivurugika na hadi leo yanabishaniwa. Buttigieg na Sanders wanaongoza Iowa, na wamekuwa watu wa mbele kwa sasa.
Biden , ambaye alionekana kuwa ni mgombea anayeongoza, amekuwa wa nne katika matokeo ya awali ya Iowa na aliondoka New Hampshire kabla ya matokeo kutolewa, akipendelea kuelekea South Carolina ambako ana uungwaji mkono miongoni mwa wapiga kura Wamarekani weusi.