SANTIAGO: Bwana Fujimori arejeshwa kwao kushtakiwa
22 Septemba 2007Rais wa zamani wa Peru Alberto Fujimori anatarajiwa kurejeshwa nchini mwake kutoka Chile ili kujibu mashtaka ya ufisadi na mauaji ya watu 25 wakati alipokuwa madarakani.Ndege ya polisi ilisafiri kutoka mji wa Tacna jana jioni kuelekea Santiago nchini Chile ili kumchukua Bwana Fujimori saa chache baada ya mahakama kuu nchini Chile kuagiza kurejeshwa kwake.Kiongozi huyo wa zamani anatarajiwa kuwasili Peru leo hii wakati wa mchana baada ya kuwa uhamishoni kwa miaka 7.
Bwana Fujimori aliye na umri wa miaka 69 aliyejaribu kurudi katika siasa huenda akafungwa jela kwa kipindi cha miaka 40.Mwanawe wa kike Bi Keiko Fujimori aliye mbunge nchini humo anatoa wito kwa wafuasi wake kumlaki Bwana Fujimori atakapowasili katika uwanja wa ndege wa Lima.
Makundi ya kutetea haki za binadamu na jamaa za waliopoteza maisha yao wakati wa utawala wa Fujimori wanapongeza uamuzi wa mahakama hiyo ya Chile.
Bwana Fujimori analaumiwa kuagiza kuuawa kwa wanafunzi 9 na mhadhiri mmoja katika chuo kikuu cha La Cantuta na mauaji ya watu wengine 15 katika mtaa mmoja wa Lima mwaka 91.
Mauaji hayo yalitekelezwa na kundi la mauaji la Colina la jeshi la serikali wakati uongozi wa Bwana Fujimori ulipambana na wanagambo wa Kimao.
Kiongozi huyo wa zamani aidha analaumiwa kuagiza kutekwa na kuteswa kwa wapinzani wake wa kisiasa.Mbali na mashtaka hayo ya mauaji Bwana Fujimori alipatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vya rushwa yakiwemo madai ya ubadhirifu wa dola milioni 15 pesa za umma. Bwana Fujimori alitoroka mwaka 2000 alipokabiliwa na kashfa ya rushwa.