1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SARAFU MADHUBUTI SIO BARAKA

7 Septemba 2011

Mpango wa kuiokoa sarafu ya Euro, mfumo wa malipo ya uzeeni na athari za sarafu imara ya Uswisi ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani Jumatano ya leo.

Basi tukianza na mzozo wa Euro, gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG linaandika:

"Nchi za kanda inayotumia sarafu ya Euro, zinahitaji sera ya pamoja ya fedha, yenye mfumo mmoja wa malipo ya kodi na utaratibu wa kuweka vikwazo. Sera kama hiyo ikiidhinishwa, basi itasaidia kurekebisha makosa yaliyofanywa mwanzoni, katika Mkataba wa Maastricht. Lakini kinachosikitisha ni kwamba kwa sababu ya jitahada za dharura za kuiokoa sarafu ya Euro, hata serikali ya Ujerumani na vyama vya upinzani vinashughulika zaidi na gharama za mpango huo badala ya kujitahidi kuurekebisha mfumo wenyewe. Hatua ya kuanzisha hisa za Euro au kuifukuza Ugiriki kutoka kanda ya Euro haitosaidia. Lakini hayo yote yanapaswa kujumuishwa katika mpango mzima."

Gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN likiendelea na mada hiyo hiyo, linaonya:

"Mzozo wa madeni ukizidi kuendelea au benki zikikabiliwa upya na hatari ya kufulisika, basi maafa yake hayatoweza kudhibitiwa. Wasiwasi uliopo hivi sasa katika masoko ya fedha unadhihirisha kiwango cha hatari hiyo. Kwani katika kipindi cha miezi miwili iliyopita tu, masoko ya fedha yalipata hasara ya Euro bilioni 5,000 baada ya thamani ya hisa kuporomoka kwa kiwango kikubwa. Na kinachovunja moyo zaidi na hata kughadhibisha, ni kwamba mzozo wa fedha uliibuka miaka mitatu iliyopita na ni miaka miwili tangu Ugiriki kufichua matatizo yake ya madeni. Na wakati huo wote, viongozi hawakuweza kupata ufumbuzi wa kumaliza matatizo hayo au kukubaliana njia ya kuzuia hali kama hiyo kutokea tena katika siku zijazo."

Wakati nchi za kanda ya Euro zikiwa mbioni kuiokoa sarafu yao, Uswisi ina tataizo jingine kabisa. Sarafu yake ya Frank ni madhubuti. Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linasema:

"Hiyo si baraka, bali ni nuksi kwani sasa,bidhaa zake ni ghali sana na hiyo imeathiri mauzo yake katika nchi za nje. Nafasi nyingi za ajira zipo hatarini."

Na gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo, linasema:

"Baadhi ya wapinzani wa sarafu ya Euro wangependa tena kuwa na sarafu ya D-Mark. Lakini kile kitakachotokea iwapo viongozi watauitikia mwito huo, kinashuhudiwa nchini Uswisi. Kwani sekta za biashara na utalii zinaathirika. Hayo ndio yatakayotokea Ujerumani, sarafu ya D-Mark ikirejeshwa, kwani wawekezaji watanunua sarafu hiyo kwa wingi na thamani yake itaongezeka sana kama ilivyotokea na sarafu ya Frank nchini Uswisi. Kwa hivyo, hata Ujerumani inayotegemea mauzo yake, itaathirika kwani bidhaa zake zitakuwa ghali sana katika nchi za nje."

Mada nyingine iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii, inahusika na malipo ya uzeeni. Gazeti la LUDWIGSBURGER KREISZEITUNG linasema:

"Mfumo mzima wa malipo ya uzeeni unapaswa kuchunguzwa upya. Na suala moja la kuulizwa ni iwapo ni busara kuweka kando sehemu ya fedha zinazolipwa na waajiriwa kwa malipo ya uzeeni, katika mfuko maalum ili kupunguza gharama. Fedha zaidi katika amfuko huo zingesaidia kupambana na matatizo ya pensheni ndogo. Anaepinga mageuzi ya kimsingi akumbuke kuwa anautia hatarini mfumo wa pensheni. Lakini ni shida kumueleza hilo mtu aliekuwa akipokea mshahara mdogo na aliefanya kazi wakati wote, na hatimae uzeeni huishia kuhitaji msaada. Bila shaka hilo ni suala tete linaloikabili serikali na linalohitaji kujadiliwa."

Mwandishi: Martin,Prema/dpa

Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW