Mullally: Mwanamke wa kwanza kuongoza Kanisa la England
3 Oktoba 2025
Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 1,400 ya Kanisa la England, mwanamke ameteuliwa kuongoza taasisi hiyo. Sarah Mullally, aliyekuwa Askofu wa London tangu mwaka 2018, amechaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury.
Mullally, mwenye umri wa miaka 63 na aliyewahi kuwa muuguzi bingwa wa saratani na Afisa Mkuu wa Uuguzi wa Uingereza, sasa atakuwa kiongozi wa kiroho wa Waanglikana zaidi ya milioni 85 duniani kote.
Uteuzi wake umekaribishwa kama hatua ya kihistoria, lakini pia umekosolewa vikali na makundi ya kihafidhina ya Waanglikana hasa kutoka Afrika, yanayopinga uongozi wa wanawake na masuala ya haki za LGBTQ.
Katika hotuba yake ya kwanza ndani ya Kanisa Kuu la Canterbury, Mullally alilaani vikali kashfa za kingono na za usalama wa kanisa, pamoja na chuki dhidi ya Wayahudi kufuatia shambulio la sinagogi huko Manchester lililoacha vifo.
"Ahadi yangu ni kuhakikisha tunasikiliza manusura, tunalinda walio hatarini, na kujenga utamaduni wa usalama na ustawi kwa wote,” alisema Mullally, akiahidi mageuzi ya kina ya ulinzi wa watoto na waumini.
Changamoto kubwa zinazomkabili
Kanisa la England limekosa kiongozi tangu Novemba mwaka jana, baada ya Justin Welby kujiuzulu kufuatia ripoti ya kuficha kashfa ya unyanyasaji wa watoto. Mullally sasa anakabiliwa na jukumu la kurejesha imani kwa waumini.
Wachambuzi wanasema changamoto kubwa zitakuwa kuporomoka kwa idadi ya waumini, malumbano ya makasisi kuhusu masuala ya kijinsia, pamoja na wito wa mageuzi ya usimamizi wa kanisa.
Linda Woodhead, profesa wa teolojia katika Chuo cha King's College London, alisema: "Uongozi wake wa upole na nguvu ni kile hasa kinachohitajika kwa wakati huu mgumu kwa kanisa na taifa.”
Mullally pia anajulikana kwa msimamo wake wa kiliberali, akiwahi kuunga mkono baraka kwa wanandoa wa jinsia moja na kushiriki katika mijadala ya kijamii kuhusu haki, afya na usawa.
Katika hotuba yake, alisema dunia ya leo "inahisi kuwa iko ukingoni,” lakini imani ya Kikristo inampa tumaini kwamba kanisa linaweza kuwa sauti ya mshikamano na haki.
Historia na nafasi yake ya kipekee
Mullally alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kuteuliwa maaskofu mnamo mwaka 2015, hatua iliyofungua njia kwa uteuzi wake wa sasa. Anafuata wanaume 105 waliowahi kushika nafasi hiyo tangu Augustine mwaka 597.
Amesema nafasi hii ni heshima kubwa na shukrani zake ni kwa wanawake waliomtangulia katika safari ya kufanikisha uongozi wa kijinsia sawa ndani ya kanisa.
"Sitakuwa sahihi kila mara, lakini nafarijika na maneno ya zaburi kwamba hata ukijikwaa, hutanguka kabisa, maana Mungu anashika mkono wako,” alisema.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alimtakia kila la heri na kusema Askofu Mkuu wa Canterbury ataendelea kuwa na nafasi muhimu katika maisha ya kitaifa. Pia Mfalme Charles III alibariki uteuzi huo.
Mullally atawekwa rasmi katika Kanisa Kuu la Canterbury Machi 2026, kwenye ibada inayotarajiwa kushuhudiwa na familia ya kifalme. Safari yake ya kihistoria inabeba matumaini mapya kwa Kanisa la England, hata kama changamoto zake ni kubwa.