1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy apewa nafasi ndogo zaidi ya kushinda uchaguzi

18 Aprili 2012

Maoni ya wapiga kura yanaonyesha kwamba Rais Nicolas Sarkozy wa nchi hiyo atapata kura chache kuliko mpinzani wake Francois Hollande katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Rais Nicolas Sarkozy katika kampeni
Rais Nicolas Sarkozy katika kampeniPicha: Reuters

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa aliupuuza utafiti wa maoni ya wapiga kura yanayoonyesha kwamba yeye atapata asilimia 24 tu ya kura zitakazopigwa Jumapili hii na hivyo kumpa ushindi mpinzani wake wa karibu Francois Hollande ambaye anatarajiwa kupata asilimia 29 ya kura. Takwimu hizo zimetolewa na shirika la kukusanya maoni ya wapiga kura liitwalo CSA. Akizungumza katika kituo cha televisheni cha BFM cha Ufaransa, Sarkozy alieleza kwamba maoni ya shirika la CSA ni tofauti kabisa na maoni yanayotolewa na mashirika mengine ambayo yote yanatabiri kwamba yeye ndiye atakayeshinda.

Mahesabu ya shirika la CSA yanaonyesha pia kwamba Francois Hollande atapata asilimia 58 ya kura katika duru ya pili ya uchaguzi huku Sarkozy akiambulia asimia 42 tu. Sarkozy hakuonekana kushtushwa na taarifa hizo. Akiendelea na kampeni zake leo, rais huyo aliwaambia watu wanaomuunga mkono wasubiri tu hadi siku ya uchaguzi ndipo waone matokeo halisi. Hata hivyo, Sarkozy sasa anaonyesha kuchoka.

Mgombea wa urais Francois HollandePicha: Reuters

Washirika wa Sarkozy wasema watampigia kura Hollande

Hapo jana Sarkozy alilitembelea eneo la Brittany ambalo kwa kawaida lina wafuasi wengi wa chama cha Kisoshalisti cha Francois Hollande. Gazeti la Le Figaro la Ufaransa, ambalo linaziunga mkono siasa za serikali, limeandika kwamba Sarkozy alionekana kutokuwa na mashaka yoyote alipolitembelea eneo la Brittany. Gazeti hilo limetabiri kwamba patakuwa na matokeo ya kustaajabisha na ambayo hayakutarajiwa siku hiyo ya Jumapili.

Mwezi uliopita maoni ya wapiga kura yalionyesha kwamba Sarkozy, anayetilia sana mkazo masuala ya usalama, atapata kura nyingi zaidi kuliko mpinzani wake Hollande. Hii ilikuwa wakati ambapo Mohammed Merah aliwaua watu saba katika miji ya Toulouse na Mountaban. Mmoja wa watu wanaofanya kazi pamoja na Sarkozy, ameliambia gazeti la Liberation, linaloegemea zaidi siasa za mrengo wa kushoto, kwamba ni lazima Sarkozy ashinde katika duru ya kwanza ya uchaguzi, la sivyo haitawezekana tena kuchukua ushindi.

Mabango ya kampeni za uchaguziPicha: dapd

Washirika wengi wa Sarkozy sasa wamegeuka na kusema kwamba watampigia Francois Hollande. Miongoni mwao ni Fadela Amara aliyekuwa naibu waziri wa mipango miji, kamishna wa zamani wa masuala ya vijana Martina Hirsch pamoja na Brigitte Girardin ambaye alikuwa waziri katika serikali ya rais wa zamani wa Ufaransa, Jaques Chirac.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman