1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaume ruksa kuwasindikiza wanawake leba Tanzania

Veronica Natalis
4 Juni 2024

Hospitali ya rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC iliyopo mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, imezindua wodi maalumu za kisasa zinazoruhusu mwanamke mjamzito kujifungua huku akiwa na mwenza wake pembeni.

Waziri wa afya Tanzania Ummy Mwalimu
Waziri wa afya Tanzania Ummy MwalimuPicha: picture-alliance/Photoshot

Mwenza huwa na sehemu maalumu ya kukaa huku amevaa vifaa maalumu vya kufatilia mapigo ya moyo ya mama na kushuhudia  mchakato mzima wa kujifungua.

Hospitali hiyo inasema uzinduzi wa wodi hizo unafuatia utafiti uliofanywa unaoonesha kuwa wanawake wanaojifungua huku wakiwa karibu na wenza wao huwa salama zaidi.
 
Maboresho yaliyofanywa katika wodi hiyo ya wazazi yanazingatia mfumo wa utolewaji wa huduma za tiba kwa mama mjamzito pamoja na huduma za kujifungua.

Soma pia:Wito watolewa kukabili vifo vya wajawazito na watoto Afrika

Kadhalika maboresho hayo, yanazingatia upendo na faragha pamoja na huduma ya kisasa ya kumkaribisha mwenza wa mama anayejifungua kushuhudia mchakato mzima. 

Kwenye wodi hiyo ya kisasa, kuna kitanda na kifaa kilichounganishwa na mfumo wa kompyuta chenye uwezo wa kufuatilia mwenendo wa mapigo ya moyo ya mtoto akiwa  bado yupo tumboni, pamoja na kiwango cha uchungu kwa mwanamke mjamzito.

Mbinu yalenga kupunguza vifo 

Pamoja na mambo mengine, mbinu hii inaelezwa kuwa imelenga kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Aidha hospitali hiyo ya KCMC inasema tafiti zinaonesha kuwa mwanamke mjamzito huwa katika hali salama zaidi endapo atajifungua huku akiwa na mwenza wake karibu.

Unaifahamu huduma ya M-Mama?

02:56

This browser does not support the video element.

Kiwango cha vifo vya uzazi nchini Tanzania ni kipimo cha idadi ya vifo vya wanawake kwa kila watoto laki moja wanaozaliwa hai. 

Soma pia:Vifo kwa wajawazito ni changamoto Tanzania

Kwa mujibu wa ripoti mbali mbali za mwaka 2022 ikiwepo ripoti ya wizara ya afya nchini Tanzania kuhusu vifo vya wanawake wanaojifungua, Idadi ya kiwango cha vifo vya uzazi nchini Tanzania ni 104, kwa kila vizazi hai laki moja.

Hata hivyo inaelezwa kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa za kupunguza vifo vya uzazi kwa kuboresha huduma za afya.

Profesa Gilierd Masenga ni mkurugenzi wa hospitali ya KCMC, amesifu mpango huo ambao utawaleta pamoja wazazi wakati wa kuleta uhai mpya duniani.

Wanufaika wausifu mpango huo

Mkunga mtaalamu akimsaidia mama kujifunguaPicha: Zigoto Tchaya

Huduma hiyo kwa sasa imekwisha anza kutolewa katika wodi ya wazazi ya kisasa ya KCMC.

Baadhi ya wakaazi wa eneo hilo ambao wamenufaika na huduma hiyo wanasema, inaongeza upendo miongoni mwa wazazi, lakini pia inamuonesha baba uhalisia wa mwanamke mjamzito anachopitia katika wakati huo.

Soma pia:UNFPA-Mamilioni ya wanawake na wasichana hawana maamuzi na miili yao

Nemes Fidel, ameshuhudia mke wake akijifungua mtoto wa kiume usiku wa kuamkia Mei 29 mwaka huu 2024, anasema amefarijika kuwa na mke katika wakati huo
 
Kulingana na shirika la Afya duniani WHO, takribani asilimia 95 ya vifo vya uzazi hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati na vingi vinaweza kuzuilika.