1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia mwenyeji wa mkutano wa mataifa ya G20

20 Novemba 2020

Wakati Saudi Arabia taifa linalosafirisha mafuta kwa wingi duniani na mshirika wa karibu wa Marekani ilipochukua urais wa kundi la mataifa tajiri duniani G20 mwaka 2019, matumaini katika taifa hilo yalikuwa makubwa.

Saudi-Arabien Riad vor dem G20 Gipfel
Picha: Fayez Nureldine/AFP/Getty Images

Mkutano wa kimataifa ulitarajiwa kuiinua nchi hiyo katika viwango vya juu zaidi vya kimataifa na kuelekeza macho ya dunia katika mageuzi muhimu yalioanzishwa na kiongozi wa sasa Mohammed Bin Salman ya kulifungua zaidi taifa hilo na kuupanua uchumi wake.

Lakini matumaini hayo yalififia baada ya mkutano wa mwaka huu wa kilele wa kundi hilo la G20 kuamuliwa kuandaliwa kwa njia ya video kutokana na janga la virusi vya Corona na hili ni pigo kubwa kwa ndoto za mfalme Salman, katika mwaka uliokumbwa na mgogoro wa kiuchumi duniani kote. Robert Mogielnicki, msomi katika taasisi ya masuala ya mataifa ya Guba mjini Washington amesema ijapokuwa alilolitaka Salman haliwezi kufanikiwa kwa sasa bado anapaswa kuendelea na juhudi zake na Wasaudi ni lazima watumie nafasi ya mkutano huu ili kujinufaisha.

Mkutano wa mwaka huu ni kwa njia ya vidioPicha: Nael Shyoukhi/REUTERS

Janga la COVID 19 ni moja ya ajenda kuu ya mipango ya kundi la G20, pamoja pia na mikakati ya kudhibiti janga hilo linaloendelea kuathiri chumi za dunia. Mkutano huo pia utajadili msamaha wa madeni kwa mataifa masikini. Kwa wakati huu sifa ya Saudi Arabia imeharibiwa kufuatia mvutano uliokuwepo mwaka 2018 kufuatia mauaji ya mwandishi habari wa taifa hilo Jamal Khashoggi, vita vya Yemen na kuendelea kushikiliwa kwa wanaharakati wa kutetea haki za wanawake waliokamatwa mwaka uliopita.

Lakini kando na hayo mkutano wa mwishoni mwa Juma hili ulionekana kama nafasi ya utawala huo wa kifalme kuuza utalii wake na maeneo yake ya kustarehe.

Safari za viongozi wa juu zilikuwa zimeshapangwa katika vivutio mbali mbali vya kitalii ikiwemo mpango wa dola bilioni 500 wa mji wa Neom kutakapokuwa na balozi mbili za kigeni hii ikiwa ni kulingana na mwandishi habari wa Reuters. Hayo yote hata hivyo hayatofanyika kutokana na kwamba mkutano huo sasa utafanyika kwa njia ya video.

Mfalme Mohammed bin Salman ameshikilia urais wa kundi la G20 kama thibitisho la jukumu lake muhimu katika uchumi wa dunia. Siku ya Alhamisi Waziri wa habari nchini humo amesema kuliongoza kundi hilo na kupata majibu mazuri hasa wakati huu wa janga la corona ni fahari kubwa kwa taifa hilo tajiri kwa mafuta.

Huku hayo yakiarifiwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na baadhi ya wabunge wa jamii ya kimataifa wamelitolea mwito kundi la G20 kuususia mkutano huo kutokana na rekodi ya Saudi Arabia ya uvunjifu wa haki za binaadamu.

Maandalizi ya mwisho ya G20Picha: Fayez Nureldine/AFP/Getty Images

Wabunge wengi nchini Uingereza, Umoja wa Ulaya na Marekani wamezitaka serikali zao kuendelea kuishinikiza Saudi Arabia kuheshimu haki za binaadamu kuelekea mkutano wao wa kilele au wajiondoe kabisa katika mkutano huo. Meya wa mjini London, Paris, New York na Los Angeles wamesusia mkutano huo.

Hii leo makundi makubwa ya haki za binaadamu watafanya mkutano wao pembezoni mwa mkutano wa G20 wakijadili ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Saudi Arabia. Mkutano huo utawajumuisha wabunge wa Marekani pamoja na mchumba wa mwaandishi Habari Jamal KKhashoggi, Khashoggi na familia za wanaharakati wanaozuiliwa na serikali akiwemo Loujain al-Hathloul, aliye katika mgomo wa kula kwa zaidi ya wiki tatu akipinga hali anayopitia akiwa kizuizini.

Mapema mwezi huu balozi wa Saudi nchini Uingereza alisema utawala huo wa kifalme unafikiria kuwaachia huru wanaharakati wa kike wanaozuiliwa lakini makundi ya haki za binaadamu yalitupilia mbali tangazo hilo yakilielezea kama maneno ya kupoza tu kuelekea mkutano wa kilele wa G20.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW