1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko yanachangia katika haki za wanawake nchini humo

Admin.WagnerD2 Agosti 2019

Wanawake nchini Saudia Arabia wataweza kupata hati ya kusafiria na kusafiri nje ya taifa hilo la kifalme bila ya idhini kutoka kwa walezi wao wa kiume kutokana na amri ya kifalme.

Japan G20 Gipfel Osaka
Picha: Reuters/J. Silva

Saudi Arabia imechapisha sheria mpya mapema leo ambazo zinalegeza amri dhidi ya wanawake kwa kuruhusu raia yeyote kutuma maombi ya paspoti na kusafiri kwa njia huru na kufikisha tamati sera ya muda mrefu ya ulezi ambayo imewapa uwezo wanaume kuwadhibiti wanawake .

Amri hiyo mpya iliyochapishwa katika gazeti la Okaz nchini Saudi Arabia, inasema kuwa yeyote mwenye umri wa miaka 21 na zaidi anaweza kupata paspoti. Uamuzi huo ni mabadiliko makubwa katika mfumo wa nchi hiyo wa ulezi ambao unahitaji wanawake kupata idhini kutoka kwa jamaa mwanaume kabla ya kufanya maamuzi makubwa.

Mabadiliko hayo yanachangia pakubwa katika haki za wanawake wa Saudia katika falme hiyo.

Kwa muda mrefu, mfumo huo wa sheria umeshtumiwa kwasababu ya kuwachukulia wanawake kama watoto maisha yao yote na kuwahitaji kutafuta idhini ya mwanamume kutafuta paspoti ama kusafiri nje ya nchi. Mara nyingi mlezi wa mwanamke huyo huwa babake ama mumewe na katika visa vingine mtoto wa kiume wa mwanamke.

Mabadiliko hayo yalifurahiwa sana na raia wa Saudi Arabia kupitia mtandao wa twitter ikiwa ni pamoja na vinyago vilivyotumwa kuonyesha watu wakikimbilia katika uwanja wa ndege na mizigo huku wengine wakimpongeza mrithi wa ufalme mwenye umri wa miaka 33 anayeaminika kuchangia katika mabadiliko hayo.

Mabadiliko zaidi

Mabadiliko mengine yaliotolewa katika amri hiyo ya kifalme yanawaruhusu wanawake kusajili ndoa , talaka ama kuzaliwa kwa mtoto na pia kukabidhiwa hati rasmi ya familia .

Pia zinasema kuwa mama ama baba anaweza kuwa mlezi wa kisheria wa watoto.

Hatua ya kuweza kupata stakabadhi za familia inapunguza changamoto zinazowakabili wanawake katika kupata kitambulisho cha serikali na kuwasajili watoto shuleni.

Hata hivyo bado kuna sheria zingalipo zinazohitaji idhini ya wanaume kwa mwanamke kuachiliwa kutoka gerezani, kujitoa katika ndoa yenye dhulma ama kuolewa. Tofauti na wanaume, wanawake hawawezi kuwapa watoto wao uraia na pia kutoa idhini kwa watoto wao kuoa ama kuolewa.

Mrithi wa mfalme katika taifa hilo Mohammed bin Salman ameleta mabadiliko mengi huku akiratibu mpango makhsusi wa mabadiliko ya kiuchumi yanayowahimiza wanawake kuingia katika ajira. Yeye ndiye aliyehusika na kuonda marufuku ya wanawake kuendesha magari mwaka jana na kulegeza sheria za ubaguzi wa kijinsia.

Hata hivyo taifa hilo la kifalme na mrithi wake bado liko chini ya uchunguzi baada ya kisa cha kukamatwa kwa wanaharakati kadhaa wa kike na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW