1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yaziita benki za nje kuwekeza nchini mwake

24 Oktoba 2018

Saudi Arabia imesema kwamba haitayaadhibu mabenki ya nje yaliyosusia kongamano la kimataifa kuhusu mustakabali wa uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake wa kuuhakikishia mkusanyiko huo uliogubikwa na hisia tofauti.

Investorenkonferenz in Saudi-Arabien
Picha: Reuters/F. Al Nasser

Saudi Arabia imesema hii leo kwamba haitayaadhibu mabenki ya nje yaliyosusia kongamano la kimataifa kuhusu mustakabali wa uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake wa kuuhakikishia mkusanyiko huo uliogubikwa na hisia tofauti kutoka kila kona duniani kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi. 

Mkuu wa benki kuu ya Saudi Arabia amesema mabenki ya nje yanayosusia kongamano hilo bado yanaweza kuomba vibali vya kufanya shughuli zao katika taifa hilo lenye nguvu zaidi kiuchumi miongoni mwa mataifa ya mashariki ya kati.

Mwana mfalme Mohammed Salman, mwenye ushawishi mkubwa anatarajiwa kuhutubia kongamano hilo la kimataifa la uwekezaji baadae hii leo, katika moja ya hotuba yake iliyohusisha viongozi wa ngazi za juu zaidi tangu mmoja wa wakosoaji wake wakubwa, Jamal Khashoggi ambaye pia alikuwa ni mchangiaji kwenye gazeti la Washington Post la Marekani kuuawa mjini Instanbul, Oktoba 2.

Salman, awali alitoa hotuba fupi ya utangulizi iliyowahusisha viongozi wa ngazi za juu kuhusu mustakabali wa kimkakati wa uwekezaji wa Saudi Arabia katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, na hii leo anatarajiwa kuwa miongoni mwa wazungumzaji wa ngazi ya juu.

Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed Salman, atahutubia kongamano hilo la uwekezaji linalofanyika mjini Riyadh Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Salman anatarajiwa pia kuwa miongoni mwa jopo la wazungumzaji, sambamba na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Lebanon, Saad Hariri, ambaye hatua yake ya kujiuzulu kupitia hotuba ya televisheni akiwa Saudi Arabia mwaka jana pia iliibua minong'ono kwamba alikuwa akishikiliwa kinyume na matakwa yake.

Bado Saudi Arabia inakabiliwa na shinikizo dhidi ya mauaji ya Khashoggi.

Saudi Arabia ambayo ni muuzaji mkubwa wa mafuta inakabiliwa na ongezeko la shinikizo kufuatia mauaji ya Khashoggi katika mzozo ambao pia umeyumbisha mahusiano ya kidiplomasia kati yake na mataifa ya magharibi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyipp Erdogan ameongeza shinikizo zaidi kwa taifa hilo hii leo, kabla hata mwana mfalme huyo wa Saudia hajahutubia kongamano hilo mjini Riyadh.

Akiwa mjini Ankara, Erdogan, amesema wanataraji mauaji hayo hayatafunikwa na wale waliohusika kuanzia mtu aliyetoa amri hadi wale waliomuua, watakabiliwa na mkono wa sheria. Hata hivyo baadae ilielezwa kuwa viongozi hao walijadili suala hilo kwa njia ya simu.

Wachumi wanasema Saudi Arabia itahitaji matrilioni ya dola kwenye uwekezaji ili kutengeneza mamilioni ya ajira kwa vijana wa taifa hilo wanaofikia umri wa kufanya kazi miaka michache ijayo. Kongamano hilo linalenga kuvutia wawekezaji kusaidia kubeba mzigo wa jitihada hizo.

Wengi wa wanasiasa wa magharibi wamesusia kongamano hilo la uwekezaji lililofunguliwa mjini Riyadh hapo jana, lakini taifa hilo la kifalme lilionyesha kuwa bado linaweza kufanya biashara kwa kusaini mikataba ya thamani ya dola bilioni 50 katika siku ya kwanza ya kongamano.

 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW