HRW: Ukiukaji wa haki unaendelea duniani ila kuna matumaini
17 Januari 2019Ripoti hiyo pia inazikosoa nchi za Ulaya. Lakini Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Ujerumani Wenzel Michalski anasema licha ya yote hayo kuna sababu ya kuwa na matumaini kidogo.
Shirika la Human Rights Watch limekuwa likichapisha ripoti hiyo kila mwaka tangu mwaka 1989. Mataifa yenye uongozi wa kidikteta ambayo haki za watoto, wanawake na wanaume zinakiukwa ndiyo yanayolengwa. Mwaka huu kama anavyosema Wenzel Michalski wanaharakati wa haki za binadamu hawajajikita tu katika baadhi ya nchi kwa ujumla bali kwa watu binafsi.
China inajaribu kuiuza sera yake ya ukiukaji wa haki za binadamu duniani
Wenzel Michalski ambaye ni mkurugenzi wa Human Rights Watch na ambaye ana umri wa miaka 56 anasema hakuna lolote jema la kuripoti kutoka China kuhusiana na haki za binadamu, kwani haki ya kujieleza na hata mashirika ya kijamii yamekandamizwa, jambo ambalo awali lilikuwa linashuhudiwa sehemu chache tu za nchi hiyo. Kwa sasa China inafanya upelelezi wa kila kitu na hata kuwatambua watu kwa sura. Mkiurugenzi huyo anasema kwamba Rais Xi Jinping anaelekea kuwa dikteta kadri siku zinavyozidi kusonga.
Kulingana na Human Rights Watch, China inajaribu kuiuza sera yake ya ukiukaji wa haki za binadamu duniani kupitia mkakati wake wa maendeleo na uekezaji katika nchi za Ulaya, Asia na Afrika.
Mbali na China ripoti ya mwaka huu pia inamuangazia rais wa Marekani Donald Trump hasa kutokana na unyama anaowatendea wakimbizi kutoka Amerika ya Kusini.
Nchi za Ulaya pia zimo kwenyae ripoti hiyo huku uchaguzi wa Umoja wa Ulaya ukikaribia
Saudi Arabia iimeangaziwa mara mbili katika ripoti hiyo, kwanza kabisa ni kutokana na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi na pili kutokana na vita vinavyoendelea katika nchi jirani ya Yemen. Tangu mwaka 2014 vita hivyo kati ya vikosi vya Rais Abd Rabbo Mansur Hadi ambaye serikali yake inaungwa mkono na Saudi Arabia na mataifa mengine ya Uarabuni na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, vimeiharibu nchi hiyo kabisa.
Michalski anasema nchi za Ulaya pia zimemulikwa katika ripoti hiyo kwasababu ya ukiukaji wa haki za binadamu. Uchaguzi katika Umoja wa Ulaya utafanyika mwezi Mei na katika nchi zote za Umoja huo kuna vyama ambavyo vinaukataa Umoja wa Ulaya jinsi ulivyo. Anasema mfano ni chama cha AfD nchini Ujerumani, kile cha Italia cha Italian Lega, chama cha FPÖ nchini Austria, chama cha Fidesz nchini Hungary na nchini Ufaransa kuna chama chake Marine Le Pen cha National Rally mwenye kufuata siasa za mrengo wa kulia.
Lakini hasa nchini Ujerumani Michalski anasema kuna matumaini kidogo kwa kuwa unaweza kuikosoa nchi hiyo kutokana na hatua yake ya kuiuzuia silaha Saudi Arabia ila wakati huo huo, Wizara yake ya mambo ya nje pamoja na Kansela wanazungumzia suala la haki za binadamu na kushutumu ukiukaji wake.
Mwandishi: Daniel Heinrich
Tafsiri: Jacob Safari
Mhariri: Caro Robi