Saudia: Tuna haki ya kuishambulia kijeshi Iran
19 Machi 2026
Hii ni kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya mataifa ya Ghuba. Haya yamesemwa Alhamis na waziri wa mambo ya kigeni wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan.
Taarifa hii imekuja wakati waandishi wa shirika la habari la Ufaransa AFP wamesema milipuko mikubwa zaidi imesikika mjini Riyadh usiku wa kuamkia Alhamis, baada ya mamlaka za taifa hilo la kifalme awali kusema kuwa lilizuia makombora 4 ya masafa marefu yaliyokuwa yanaelekea katika mji mkuu Riyadh.
Haya yanafanyika wakati ambapo jeshi la mapinduzi la Iran limeyaonya hayo mataifa ya Ghuba kwamba viwanda vyao vya mafuta na gesi vitashambuliwa na "kuharibiwa kabisa" iwapo Israel na Marekani watafanya mashambulizi zaidi dhidi ya miundo mbinu ya nishati ya Iran.
Maafisa wa Iran watimuliwa Qatar
Katika taarifa, jeshi hilo limesema jawabu lake litakuwa kubwa kuliko shambulizi ililofanya katika kituo kikubwa zaidi cha gesi duniani kilichoko Qatar, cha Ras Laffan. Awali Iran ilikuwa imeilaumu Marekani na Israel kwa mashambulizi katika kituo chake kikubwa cha gesi cha South Pars.
Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar walikuwa wametoa taarifa mbalimbali kulaani mashambulizi hayo katika kiwanda cha gesi cha Iran.
Wakati hayo yakijiri, Qatar kupitia wizara yake ya mambo ya nje imewaagiza maafisa wa jeshi na usalama wa Iran kuondoka nchini humo katika kipindi cha saa 24 zijazo. Qatar imechukua hatua hiyo kufuatia kushambuliwa kwa kituo chake cha gesi cha Ras Laffan.
Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X amesema amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na Emir wa Qatar na kuwataka kutoa amri ya kusitishwa kwa mashambulizi katika miundo mbinu ya kiraia hasa miundo mbinu ya nishati na maji.
Na mashambulizi ya usiku kucha ya Iran yamesababisha kifo cha mtu mmoja aliyetambulishwa kama mfanyakazi wa kigeni karibu kilomita 20 kaskazini mashariki mwa Tel Aviv huko Israel. Haya yamethibitishwa na madaktari wa Israel na kupelekea idadi ya waliofariki nchini humo kutokana na vita hivyo kufikia watu 15.
Wakati huo huo wanawake watatu wa Kipalestina wameuwawa katika Ukingo wa Magharibi baada ya kuangukiwa na mabaki ya makombora, muda mfupi baada ya Israel kutangaza msururu wa mashambulizi ya makombora ya Iran.
Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililofanyika karibu na eneo la hebron, akiwemo mwanamke aliyekuwa hali mahututi baada ya kuripotiwa awali kuwa alikuwa amefariki. Haya ni kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Palestina. Hivi ndivyo vifo vya kwanza vya Wapalestina kuripotiwa huku vita hivyo vikiendelea.
Kisasi kulipizwa kwa wauwaji wa Larijani
Haya yanafanyika wakati ambapo Kuwait imesema kuwa imewakata wanamgambo 10 walio na mafungamano na kundi la wanamgambo la Lebanon la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran. Kuwait kupitia wizara yake ya usalama wa ndani imesema wanamgambo hao walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miundo mbinu muhimu.
Naye kiongozi mpya mkuu wa Iran Ayatollah Mojtaba Khamenei ametoa taarifa yake ya pili tangu kuanza kwa vita hivyo akisema wauwaji wa mkuu wa usalama wa nchi hiyo Ali Larijani ni sharti watalipa kwa shambulizi hilo. Mojtaba Khamenei hajaonekana hadharani tangu achukue mamlaka baada ya kuuwawa kwa babake Ayatollah Ali Khamenei.
Taarifa hii ya Mojtaba Khamenei imetolewa huku jeshi la Israel likiapa kuendelea na mashambulizi ya kuwalenga maafisa wa serikali ya Iran, baada ya kutangaza kumuua waziri wa ujasusi Esmail Khatib.
Wakati huo huo mamlaka kote katika mataifa ya Ghuba zimetangaza kuwa ibada za sikukuu ya Iddi ambayo inaashiria mwisho wa mwezi wa mfungo wa Ramadhan, zitafanyika ndani ya misikiti ya kawaida badala ya kufanyika nje ambapo kwa kawaida maelfu ya waumini hukusanyika kuadhimisha sikukuu hiyo. Mataifa hayo yamesema hatua hiyo ni ya tahadhari.
Vyanzo: Reuters/AFP