1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yaifungulia mipaka Qatar kupunguza mivutano ya Ghuba

Daniel Gakuba
5 Januari 2021

Wakati viongozi wa nchi za Ghuba ya Uarabu wakifanya mkutano wao wa kilele leo, Saudi Arabia imeifungulia mipaka ya anga na ardhini Qatar, katika ishara ya kupunguza uhasama wa zaidi ya miaka mitatu katika ukanda huo.

Katar, Doha I Qatari Emir Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani und  Sheikh Ahmad Nasser al-Sabah
Kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani (kushoto) katika mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Kuwait, Sheikh Ahmad Nasser al-Sabah. (Picha ya Maktaba)Picha: Qatari Emirate Council/AA/picture alliance

Taarifa kwamba Saudia Arabia itaifungulia mipaka Qatar zimetangazwa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Kuwait jana jioni, ambayo imeeleza kuwa kuanzia jioni ya jana Jumatatu, mipaka ya anga, nchi kavu na bahari kati ya Saudi Arabia na Qatar itakuwa wazi kwa mara ya kwanza tangu katikati mwa mwaka 2017.

Soma zaidi: Mataifa ya Ghuba yako tayari kuzungumza na Qatar

Waziri wa mambo ya nje wa Kuwait  Ahmed Nasser al-Mohammed al-Sabah amesema Kiongozi wa Kuwait,  Nawaf al-Ahmed al-Sabah ndiye ametowa mapendekezo yaliyosaidia kufunguliwa tena kwa mipaka baina ya Saudi Arabia na Qatar, katika mazungumzo aliyoyafanya na mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.

Qatar imetengwa katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba tangu mwaka 2017Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Nabil

''Katika mazungumzo hayo imehakikishwa na kusisitizwa kuwa kila upande unataka muungano na kwa kauli moja wanataka kusaini ilani ya al-Ula, ambayo itafungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kidugu usio na vizingiti,'' amesema waziri huyo na kuongeza kuwa  ''kulingana na mapendekezo ya kiongozi wa Kuwait Nawaf Ahmad al-Sabah, imeamuliwa kuwa mipaka ya angani, ya ardhini na ya baharini kati ya Saudi Arabia na Qatar kuanzia usiku huu.''

Tuhuma za kusaidia makundi ya itikadi kali

Kuwait na Marekani zimekuwa zikifanya juhudi kuusuluhisha mgogoro wa Ghuba ya Uarabu, kati ya Qatar kwa upande mmoja na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri  kwa upande mwingine, ambazo zimeitenga Qatar kwa muda wa miaka zaidi ya mitatu iliyopita, zikiituhumu kufadhili makundi ya itikadi kali za kiislamu, na kuwa na mahusiano ya karibu na Iran.

Mfalme wa Saudi Arabia, Salman (aliyekaa) na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Mohammed bin Salman ndio wenyeji wa mkutano wa leoPicha: picture-alliance/AP Photo

Nchi ndogo ya Qatar inao mpaka wa ardhi na Saudi Arabia pekee, na ilikuwa ikiutegemea mpaka huo kwa usafirishaji wa bidhaa muhimu za vyakula na za ujenzi, na tangu mwaka 2017 umefunguliwa kwa muda mfupi tu kuruhusu mahujaji kwenda nchini Saudi Arabia.

Soma zaidi: Qatar yasikitishwa na Uamuzi mpya wa nchi nne zinazoisusia

Haikubainika mara moja Qatar imezitoa ahadi gani katika kuridhia masharti iliyokuwa imewekewa na majirani zake, ambayo ni pamoja na kukifunga kituo cha televisheni cha Al-Jazeera na kupunguza kukaribiana na Iran.

Bado njia haijanyooka 

Ingawa Saudi Arabia inaonekana kulegeza msimamo katika mzozo huo, kutanzuliwa kwake hakuko karibu kwa sababu tofauti kubwa zaidi zinasalia baina ya Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo zina tofautiana sana kisera.

Kufuatia tangazo la Kuwait la kufunguliwa kwa mipaka baina yaSaudi Arabia na Qatar, naibu waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Anwar Gargash amesema kupitia mtandao wa twitter, kwamba ''Umoja wa Falme za Kiarabu inao pia utashi wa kurejesha umoja katika ukanda wa ghuba, '' ila akatahadharisha kwamba ''bado yapo mengi ya kufanyia kazi.''

Qatar imethibitisha kuwa kiongozi wake mkuu Tamim bin Hamad al-Thani atashiriki katika mkutano wa kilele wa Ghuba nchini Saudi Arabia, ambao utahudhuriwa pia na Jared Kushner, mkwe wa rais Donald Trump ambaye pia ni mshauri wake.

ape, rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW