1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yapinga lawama za mauaji ya watoto Yemen

5 Juni 2016

Muungano unaongozwa na Saudi Arabia unaopambana na waasi wa Kihuthi Yemen Jumapili (05.06.2016) umeikataa repoti ya Umoja wa Mataifa iliouweka kwenye orodha mbaya kutokana na vifo vya watoto katika mashambulizi ya anga.

Picha: Reuters/Mohamed al-Sayaghi

Muungano unaongozwa na Saudi Arabia unaopambana na waasi wa jamii ya Kihuthi nchini Yemen Jumapili (05.06.2016) umeikataa repoti ya Umoja wa Mataifa ambayo imeuweka kwenye orodha mbaya kutokana na vifo vya watoto katika mashambulizi ya anga yanayofanywa na kundi hilo.

Generali Ahmed Assiri ameliambia shirika la habari la serikali nchini Saudi Arabia la Saudi Press Agency kwamba repoti hiyo haina urari na takwimu zake sio za kuaminika na wala haiwezi kuwasaidia wananchi wa Yemen.

Amesema kwamba inaupotosha umma kwa kutaja idadi isio sahihi na kwa kutegemea takriban taarifa zote kutoka duru zenye uhusiano na wanamgambo wa Kihuthi na rais wa zamani aliyeondolewa madarakani Ali Abdallah Saleh.

Repoti hiyo iliyotolewa Alhamisi na ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon imesema watoto 785 wameuwawa na wengjne 1,168 wamejeruhiwa nchini Yemen mwaka jana ikiulaumu muungano huo unaongozwa na Saudi Arabia kwa kuhusika na maafa hayo.

Umoja wa Mataifa imeuweka kwenye orodha mbaya muungano huo pamoja na vlkosi vya waasi kwa ukiukaji mkubwa sana wa haki za binaadamu ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya shule na hospitali.

Inachofanya Saudia nchini Yemen

Saudi Arabia ilianzisha operesheni ya mashambulizi ya anga nchini Yemen hapo mwezi wa Machi mwaka jana kuisaidia serikali ya Rais Mansur Abedrabbo Hadi inayotambuliwa kimataifa kupambana na waasi wa Huthi wanaotuhumiwa kuwa na mafungamano na Iran na vikosi vya kijeshi vilio tiifu kwa Saleh ambaye alitimuliwa madarakani hapo mwaka 2012 kuzingatia makubaliano yaliosimamiwa na mataifa ya Ghuba.

Wanajeshi wa muungano unaongozwa na Saudi Arabia katika doria Aden.Picha: Reuters/Faisal Al Nasser

Assiri amesema " muungano huo unaongozwa na Saudi Arabia uko nchini Yemen kuwalinda wananchi wa Yemen wakiwemo watoto kutokana na vitendo vya wanamgambo wa Kihuthi."

Ametowa mfano wa mpango wa msaada wa dola milioni 30 kwa ajili ya Yemen uliozinduliwa kwa ushirikiano na Shirika la Kuhudumiwa Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Repoti haina tija kwa mazungumzo ya amani

Katika matamshi tafauti aliyoyatowa katika gazeti litolewalo kila siku nchini Saudi Arabia la Al-Sharq Al-Aswat amesema repoti hiyo ya Ban haitosaidia mazungumzo ya amani yanayoendelea kufanyika nchini Kuwait na itafanya shughuli ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Sheik kuzidi kuwa ngumu.

Mvulana mabegani mwa baba yake katika maandamano ya Wahuthi kupinga mashambulizi ya Saudi Arabia katika mji mkuu wa Sanaa.Picha: Reuters

Mashirika ya kutetea haki za biaadamu mara kwa mara yamekuwa yakielezea wasi wasi wao kuhusu mashambulizi ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia katika maeneo ya miji nchini Yemen na kuushutumu muungano huo kwa kuwalenga raia kwa makusudi katika mashambulizi yao ya mabomu ya mtawanyo jambo ambalo linamaanisha uhalifu wa vita.

Mwishoni mwa mwezi wa Mei jarida la Marekani la Sera ya Kigeni limeripotiwa kwamba Ikulu ya Marekani imesitisha shehena ya mabomu hayo kupelekwa Saudi Arabia kutokana na wasi wasi kwamba mshirika wake huyo katika Ghuba anayatumia katika maeneo ambapo kuna raia.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa vita vya Yemen vimepelekea kuuwawa kwa watu 6,400.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Iddi Sessanga