Saudia yasema ardhi yake haitotumika kuishambulia Iran
28 Januari 2026
Hayo yameripotiwa na Shirika la Habari la Saudi Arabia - SPA, likinukuu sehemu ya mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa shirika la SPA, Mwanamfalme Bin Salman -- ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia -- amemweleza Rais Pezeshkian kuwa utawala mjini Riyadh unaheshimu uhuru na hadhi ya mipaka ya Iran, na kwamba kamwe ardhi ya Saudi Arabia haitotumika kutekeleza shambulizi lolote la kijeshi dhidi ya Tehran.
Matamshi ya Bin Salman yameripotiwa katika wakati kuna wasiwasi kwamba Marekani inaweza kuishambulia Iran baada ya kuituhumu serikali ya nchi hiyo kufanya mauaji na ukandamizaji kwa maandamano ya umma yalitokea mapema mwezi huu.